Hatima ya bajeti leo, wabunge kupigia kura

WABUNGE leo watapiga kura kupitisha Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka 2023/24 baada ya kuijadili kwa siku saba.

Serikali iliwasililisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya serikali ya Sh trilioni 44.39 kwa mwaka 2023/24 ikiwa na vipaumbele kadhaa vikiwamo vya ukamilishaji wa miradi ya kielelezo ya kimkakati.

Miradi hiyo ni ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), uboreshaji wa Shirika la Ndege (ATCL) na mradi wa kuchakata na kusindika gesi asilia NLG.

Pia ukamilishaji wa mradi wa Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere na miradi minginie ya kufua umeme wa maji, ujenzi wa Daraja la JP Magufuli (Kigongo-Busisi), ujenzi wa barabara na madaraja makubwa kwa lengo la kuchochea uchumi.

Wakichangia wabunge wameishauri Serikali kuendelea kuimarisha na kuwekeza kwenye sekta ya kilimo ili kukuza uchumi huku wakitaka eneo la kilimo cha umwagiliaji lipewe msukumo na uwekezaji mkubwa.

Pia wamepinga tozo ya Sh 100 kwenye lita ya mafuta petroli na dizeli kwani itachangia kuongezeka gharama za maisha na Sh 100 kwenye mfuko wa saruji kwani kutawafanya kuchelewa kupata maendeleo ya makazi bora.

Wabunge pia wameishauri serikali kuja na vyanzo vipya vya mapato badala ya kuendelea kutegemea kodi, tozo na ushuru kwenye bidhaa.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button