DAR ES SALAAM; KILA mtu aliyezaliwa anacho kitu cha pekee alichojaaliwa kuwa nacho. Kitu hiki si umbile lake, elimu yake, umaarufu wake, usomi wake, cheo chake katika jamii, au utajiri wake wa vitu na fedha; la hasha, bali ni kipaji chake.
Kipaji ni uwezo wa kiasili ulio ndani ya mtu katika maumbile, nafsi na roho yake. Kipaji kinatoka ndani yake. Ni tunu au zawadi toka kwa Mungu ambayo hakuna anayeweza kutunyang’anya au kutuibia mpaka tutakapokufa.
Fedha na magari vyaweza kuibiwa, nyumba inaweza kuanguka, kubomoka, kubomolewa au hata kuungua, lakini vipaji hubakia kuwa nasi daima.
Isome:https://habarileo.co.tz/mzumbe-wandaa-tamasha-kuibua-vipaji/
Kipaji ni karama. Ni zawadi anayokirimiwa mtu kutoka kwa Mungu. Kipaji hiki hukua katika ufanisi na matumizi ikiwa kitakuzwa na kuendelezwa na kimenuiwa kutumika kwa niaba ya vingine, si kwa ajili ya ubinafsi bali kwa faida ya wengine na si yake mwenyewe.
Kwa kawaida kila mtu ameletwa duniani kwa kusudi maalumu na la kipekee. Ili kutekeleza kusudi hilo, Mungu katujaalia vipaji mbalimbali, wengine wamepewa vipaji vya uimbaji, uigizaji, ufundi, uchoraji, uchongaji, ususi, uchezaji muziki, uchekeshaji, uchezaji michezo mbalimbali, ujasiriamali, utabibu, ualimu, uongozi katika jamii, ugunduzi, uandishi n.k.
Wapo watu wanaolalamikiwa au kulaumiwa kuwa hawana ubunifu. Lakini kila mtu ana upekee katika jamii kupitia kipaji chake. Hakuna mtu yeyote yule mwenye afya njema asiye na kipaji, ni kwa vile tumeshindwa kukitambua kipaji chake.
Kwa kifupi, wengi wetu tunashindwa kabisa kuvitambua, kuviendeleza na kuvitunza vipaji vyetu. Unaweza ukawa unazunguka kila kona kutafuta ajira, kumbe unatembea na ajira au mtaji wako ambao labda ni sauti yako nzuri kwa kuimba.
Ni muhimu sana kutambua kipaji chako ambacho ni mtaji wa kukupa ajira. Ukitambua kipaji chako na kukitumia ipasavyo utakuja kuwa mtu muhimu sana katika jamii. Hebu fikiria mtu kama Nasib Abdul almaarufu Diamond Platnumz au Ali Kiba, hivi wangebaki kulalamika kwa kuwa hawajafika chuo kikuu au wangetegemea kuajiriwa ingekuwaje leo!
Wengi tunaojiona tumesoma au tuna utaalamu hatuufikii utajiri wa Diamond Platinumz, kwani kipaji chake cha kuimba kimemfanya amiliki miradi ya maana.
Isome pia:https://habarileo.co.tz/mfumo-kupima-vipaji-vya-watoto-wazinduliwa/
Leo hii watu kama Diamond, vipaji vyao vimekuwa msaada hata kwa watu wengine wakiwemo jamaa zao na watu wanaowazunguka. Ni vipaji ambavyo tunazaliwa navyo kwa ajili ya faida ya mwenye kipaji na jamii nzima.
Mtu anapewa kipawa cha asili kama matokeo ya mchanganyiko wa jenetiki (huweza kurithiwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine), baadhi wakiwa na uwezo wa asili katika muziki, sanaa, au hisabati.
Pia kinaweza kutokana na mazingira (endapo utakulia katika familia ya muziki itachangia katika kuendeleza kipaji cha muziki). Lakini ili kipaji kifanye kazi yake sawasawa kwa kusudi la Mungu ni lazima mtu atumie kipaji chake kwa lengo la kuisaidia jamii yake.
Ni kama nyuki wanavyotengeneza asali tamu na ya ubora wa viwango vya hali ya juu, lakini hawafundishwi na yeyote wala kusomea popote. Hawana cheti wala shahada ya chuo kikuu bali ni uwezo wa asili ulio ndani yao.
Ndivyo vipaji vyetu vilivyo, ni kama uwezo wa nyuki ulivyo katika kuzalisha asali tamu. Lakini vipaji hivi vinatofautiana kati ya mtu na mtu, kutokana na jinsi vilivyokuzwa na kuendelezwa.
Watu wanapewa vipawa ili waweze kusaidia kuchangia maendeleo kwenye jamii zao, na kama kipaji alichopewa mtu hakitumiki ipasavyo ni sawa na kumiliki bunduki bila risasi halafu utegemee utaitumia bunduki hiyo kuwindia au kujilinda.
Isome pia:https://habarileo.co.tz/vyombo-vya-ulinzi-vyatakiwa-kuibua-vipaji-shuleni/
Kwa kutumia vipaji vyetu ipasavyo, sisi pia hupata ukamilifu katika maisha kupitia kwa kazi zetu. Kwa mfano, mimi kama mwandishi ili niweze kuwa mkamilifu ni lazima niandike mambo yanayoigusa na kuisaidia jamii yangu.
Ndiyo, uandishi ni kipaji, mwandishi mzuri lazima kwanza awe na kipaji na uwezo wa kuandika kabla hajasomea. Hapo utagundua kuwa kipaji mtu huzaliwa nacho au hukipata katika umri mdogo, hasa kutokana na mazingira anayokulia.
Lakini kipaji hiki kinapaswa kuendelezwa kwa mafunzo au kutumika kwa muda mrefu ili aliyejaaliwa kipaji hicho aweze kufanikiwa, na ukifuatilia historia ya waandishi wengi waliofanikiwa utagundua kuwa wameviendeleza vipaji vyao na kuishi muda wao mwingi katika maisha yao wakifanya kazi ya kuandika bila kuchoka.
Hivyo, ni kazi ya jamii kusaidia kuwajenga vijana wenye vipaji ili waweze kuimarika zaidi na kutumia vipaji vyao kwa ajili ya kuleta maendeleo katika nchi. Matokeo yawe kwamba vipawa hivi vitumike kulifanya taifa kuwa na nguvu za kiuchumi na kukuza ajira.
0685 666964 au bjhiluka@yahoo.com