Kabudi asifu vyombo vya habari utulivu nchini
SERIKALI imepongeza kazi iliyofanywa na vyombo vya habari nchini katika kipindi cha Uchaguzi Mkuu hadi sasa.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Palamagamba Kabudi amesema vyombo hivyo vimekuwa vikiripoti taarifa kwa umahiri na weledi.
Profesa Kabudi alisema hayo katika mkutano wa Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba mkoani Dar es Salaam na akasema vyombo vya habari ni wadau kwa kuwa vimekuwa na utulivu nchini.
SOMA: Prof. Kabudi: AI si tishio la ajira zenu
“Vyombo vya habari vimekuwa vikiripoti kwa kutambua kwamba nchi hii ni yetu na hata sisi pia,” alisema.
Profesa Kabudi alisema vyombo vya habari vimefanya kazi ya kuhakikisha kuna utulivu miongoni mwa Watanzania hasa katika kipindi cha kampeni, wakati wa uchaguzi na baada ya uchaguzi.
Awali, alisema Dk Mwigulu amekuwa rafiki na mdau wa vyombo vya habari na wanahabari wote kwa ujumla na ndio maana aliwapa kundi la wahariri kipaumbele cha mwanzo kati ya makundi mengine ya kimkakati.
“Na hii imejidhihirisha kwamba miongoni mwa makundi ya mwanzo ya kimkakati ambayo umeamua kukutana nayo ni wahariri, maana yake umeona ni kundi muhimu, la wadau na marafiki zako ambao umekuwa nao katika nyakati zote na hata sasa umeendelea kuwa nalo,” alisema Profesa Kabudi.
Katika hatua nyingine, Profesa Kabudi alisema hatua kadhaa zimechukuliwa kuhusu vyombo vya habari ikiwemo sheria ya huduma za habari imefanyiwa marekebisho na imeanza kufanya kazi na bado wanaendelea kuona maeneo yatakayotakiwa kufanyiwa kazi zaidi.
Pia, alisema imeundwa Bodi ya Ithibati ya waandishi wa habari na inafanya kazi na hadi sasa waandishi 3,200 wamepewa ithibati na kutambuliwa kufanya kazi hiyo ya kitaaluma.
Alisisitiza bodi hiyo imeundwa si kuwa chombo tu cha kudhibiti bali pia cha kulea na kukuza taaluma ya habari, akiwemo yeye kwani pamoja na kwenda kusoma sheria bado ameendelea kuwa mwandishi wa habari siku zote.



