Kamati yasisitiza usiri huduma kwa wateja

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya Ukimwi imesisitiza umuhimu wa kuzingatia usiri katika utoaji wa huduma kwa watu, hasa wenye Virusi vya Ukimwi (VVU), ili kuendelea kutimiza azma ya Serikali ya kuboresha huduma bora za afya kwa wananchi.
Hayo yamesemwa na Kaimu Mwenyekiti wa Kamati hiyo,Hassan Mtenga, wakati wa ziara yao katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara, Oktoba 11, 2024 ambapo ameupongeza uongozi wa hospitali hiyo kwa kutoa huduma bora na kwa kuzingatia faragha ya wagonjwa.
SOMA: Hospitali za rufaa mikoa kutumia Tehama
Mtenga ameridhishwa na huduma zinazotolewa na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara, hususan kwenye Kitengo cha Tiba na Matunzo kwa watu wenye Virusi vya Ukimwi (CTC) akisema kuwa utunzaji na weledi unaoonyeshwa na watumishi wa hospitali hiyo ni wa kiwango cha juu na unaakisi azma ya Serikali ya kuboresha huduma za afya nchini.
“Huduma bora na usiri ni nyenzo muhimu za kuwafanya wagonjwa kuwa na ujasiri wa kutafuta matibabu na kufuata ushauri wa madaktari bila hofu ya kubaguliwa,” amesema Mhe. Mtenga.
Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel, amebainisha kuwa usiri ni jambo la msingi katika kuhakikisha watu wanapata matibabu bila hofu ya unyanyapaa.
KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YASISITIZA USIRI WA HUDUMA KWA WATEJA
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI imesisitiza umuhimu wa kuzingatia usiri katika utoaji wa huduma kwa watu, hasa wenye Virusi vya Ukimwi (VVU), ili kuendelea kutimiza azma ya Serikali ya… pic.twitter.com/U6PDQAta6D
— Wizara ya Afya Tanzania 🇹🇿 (@wizara_afyatz) October 12, 2024