“Kamilisheni uchunguzi wizi vifaa vya hospitali”

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa ameuagiza uongozi wa Mkoa wa Mwanza kukamilisha uchunguzi wa watumishi wa Hospitali ya Wilaya ya Sengerema wanaodaiwa kuhusika na wizi wa vifaa hospitalini hapo ili watakaothibitika wachukuliwe hatua za kisheria.
Majaliwa ametoa maagizo hayo leo Mei 19, 2025 wakati akizungumza na wananchi baada ya kukagua na kuweka Jiwe la Msingi mradi wa ujenzi Hospitali ya Wilaya ya Sengerema akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Mwanza, ambapo amewasisitiza watumishi kuwahudumia wananchi ipasavyo.
SOMA ZAIDI: Majaliwa atoa maagizo kuimarisha ushirika
”Watumishi mnatakiwa kuwahudumia wananchi kwa uaminifu na uadilifu mkubwa na Serikali haitomvumilia yoyote atakayethibitika kuhusika na wizi. Ni muhimu sana kutunza vifaa, hapa tumeleta pikipiki tatu zimeibiwa, vifaa vya ujenzi na vifaa tiba vimeibiwa na matairi ya gari la wagonjwa yameibiwa mnataka litembee vipi,”amesema Majaliwa.
SOMA ZAIDI: Samia amtaka Majaliwa kufika Somanga
Amesema serikali inatoa fedha nyingi kwa ajili ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma mbalimbali zikiwemo za afya karibu na makazi yao ili kuwaondolea usumbufu na gharama za kufuata huduma hizo mbali na makazi yao, hivyo ni muhimu kutunza rasilimali hizo na watumishi wote watakaobainika kuhusika na wizi wachukuliwe hatua.