HALMASHAURI ya mji Kasulu mkoani Kigoma, imekamilisha ujenzi wa madarasa manne na mabweni mawili yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 320, ili kuruhusu kuanza kwa masomo ya kidato cha tano na sita kwenye Shule ya Sekondari Muka.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Muka, Januari Danford akizungumza shuleni hapo amesema kuwa zaidi ya Sh milioni 402 .4 zimetolewa na serikali kwa ajili ya utekelezaji wa mpango huo na kwa awamu ya kwanza wanafunzi 160 wataanza masomo mapema mwaka ujao.
Amesema kuwa katika fedha zilizotolewa kiasi cha Sh milioni 272 zimetumika kwa ujenzi wa mabweni ya kulala wanafunzi, Sh milioni 104 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa manne na Sh milioni 26.4 kwa ajili ya ujenzi wa matundu 12 ya vyoo.
Amesema kuwa utekelezaji wa mradi huo utawezesha wanafunzi katika shule za sekondari za Kambanga na Msambara kupata nafasi ya kuendelea na masoko ya kidato cha tano, kwani kabla hapo hakukuwa na shule ya aina hiyo katika eneo hilo.
Akizungumzia ujenzi wa madarasa na bweni la wanafunzi mmoja wa wananchi wa Kijiji cha Msambara, Alphoce Masunzu alisema kuwa wanafarijika kwa serikali kukamilisha mradi huo, kwani hawakuwa na shule ya sekondari ya kiwango cha kidato cha tano na sita, hivyo iliwalazimu wazazi kutumia nguvu kubwa kuwasomesha watoto wao mbali na maeneo yao.