KESI za kupinga ushindi wa Rais Mteule, William Ruto zilizowasilishwa katika Mahakama ya Upeo juzi Jumatatu, zimemuongezea Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta muda wa kubaki madarakani.
Rais Uhuru alipaswa kuondoka Ikulu Jumanne wiki ijayo, hata hivyo kwa mujibu wa Katiba ya nchi hiyo, Kifungu cha 142 (1) kinasema kuwa Rais aliye madarakani ataondoka tu iwapo mrithi wake ataapishwa.
Hatua ya mgombea urais wa Azimio la Umoja, Raila Odinga na walalamikaji wengine kwenda Mahakama ya Upeo kupinga matokeo yaliyotangazwa wiki iliyopita na Tume ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), inampa Rais Uhuru muda zaidi kukaa Ikulu.
Majaji saba wa Mahakama ya Juu – Jaji Mkuu Martha Koome, Philomena Mwilu, William Ouko, Mohammed Ibrahim, Dk Smokin Wanjala, Njoki Ndungu na Isaac Lenaola wanatarajiwa kutoa uamuzi wao Septemba 5, 2022.
Iwapo majaji hao wataamua kuwa Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9 uliendeshwa kwa njia huru na haki kwa kuzingatia Katiba na sheria zilizopo, Rais Mteule Ruto ataapishwa Septemba 12, 2022.
Lakini Rais Kenyatta ataendelea kubaki Ikulu kwa miezi miwili zaidi iwapo mahakama itabatilisha ushindi wa Dk Ruto na kuagiza IEBC kuandaa uchaguzi mpya wa urais ndani ya siku 60.
Raila Odinga amefungua kesi Mahakama ya Upeo ya kupinga matokeo ya uchaguzi na kutaka Mwenyekiti wa IEBC, Wafula Chebukati atimuliwe na kuzuiliwa kushikilia wadhifa katika ofisi ya umma. Chebukati anatarajiwa kustaafu Januari 20, 2023.