Kiduku kuwasha moto Ujerumani leo
BONDIA Twaha Kassim ‘Kiduku’ anatarajia kupanda ulingoni Leo kuchuana na bondia wa Ujerumani Juergen Doberstein katika pambano la kuwania mkanda wa kimataifa wa Baraza la Masumbwi la Dunia(GBC).
Pambano hilo la uzito wa kati linatarajiwa kupigwa katika ukumbi wa Jo Deckarm Halle, katika mji wa Saarbruecken.
SOMA: Kiduku: wamemkanyaga nyoka mkia
Wanakutana mabondia wawili wazoefu, Kiduku akiwa amecheza mapambano 34 na kati ya hayo, ameshinda 24, amepoteza tisa na kupata sare moja huku mpinzani wake akiwa amecheza mapambano 37 na kati ya hayo, ameshinda 31, amepoteza matano na kutoka sare moja.
Mara ya mwisho Kiduku alicheza pambano la Kimataifa Aprili dhidi ya bondia Harpreet Singh wa India na kushinda kwa TKO mkoani Morogoro.
Kwa mujibu wa Kiduku, amefanya maandalizi mazuri kuhakikisha anashinda na kuweka heshima ya taifa.
“Najua halitakuwa pambano rahisi, Lakini nimejipanga na niko tayari kuipigania bendera ya Tanzania,”amesema.
Mara ya mwisho Kiduku kutoka nje ya nchi ilikuwa 2021 alipokwenda Urusi kupambana na Bek Nurmaganbet na kupoteza kwa pointi.