WANANCHI mbalimbali mkoani Kigoma, Mtwara na maeneo mengine wamepongeza hatua ya serikali kutaka kuifanya Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kuwa mamlaka hatua itakayoipa uwezo na nguvu ya kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
Mmoja wa wananchi hao, Zuhura Iddy amesema NEMC ikiwa mamlaka itakuwa na nguvu ya kusimamia kikamilifu vyanzo vya maji kwani vyanzo vingi mkoani humo vimechafuliwa.
Amesema hali hiyo inaweza kusababisha magonjwa ya mlipuko wakati wa mvua za masika na kwamba watu wanaofanya shughuli za uzalishaji wa mawese wamekuwa wakiongoza kwa kuchafua mazingira.
Zuhura amesema watu hao mara nyingi wamekuwa wakikaa karibu na vyanzo vya maji kama pembeni ya mito na maziwa hasa mto Malagalasi.
“Kuna ujenzi holela ndani ya mita 60 na ndiyo maana kunakuwa na maafa yakitokea mafuriko kwasababu watu wako jirani kabisa na mto lakini NEMC ikiwa mamlaka itawaondoa hawa watu kuwaepusha na majanga,” amesema.
Aidha, amesema kuna ujenzi holela unaondelea maeneo mbalimbali ambapo watu wanajenga bila kupata vibali vya ujenzi hali inayowafanya kujenga hata pembeni ya vyanzo vya maji.
“Sisi tutafurahi kama NEMC itakuwa mamlaka kwasababu itaweza kusimamia sheria zao na itakuwa na meno na nguvu na kutakuwa na maendeleo endelevu yanayojari utunzani wa mazingira,” amesema
John Haule mkazi wa Uvinza amesema kumekuwa na shughuli nyingi za kibinadamu zinazoharibu mazingira mkoani humo na kwamba hatua ya NEMC kuwa mamlaka inaweza kudhibiti hali hiyo.
Amesema ujenzi wa ndani ya mita 60 kutoka vyanzo vya maji yamekuwa maisha ya kawaida kwa watu wenye fedha kwani wanafahamu fika kwamba NEMC haiwezi kuwashughulikia.
“Wanafanya hivi wakifahamu fika kuwa aliyewapa kibali cha ujenzi siyo NEMC na haina cha kuwafanya lakini NEMC ikija kuwa mamlaka ujenzi holela kando ya vyanzo vya maji utadhibitiwa sana kwasababu itakuwa na uwezo wa kuwatoza faini wahusika na hata kuwabomolea,” amesema
Mkazi mwingine wa Kibondo, Ibrahim Singu amesema wameshuhudia mwingiliano mkubwa wa taasisi mbalimbali katika utendaji kazi mfano ujenzi wa baa na kumbi za starehe kwenye makazi ya watu.
“Kweli kelele zikizidi huwa tunawaita NEMC ila hata hivyo hawana meno kwasababu wahusika wanapewa vibali na halmashauri kwa hiyo wananchi tunaomba serikali iipe meno NEMC iwe mamlaka ili iweze kudhibiti hali hii,” alisema
John Joseph ambaye ni mkazi wa Mtwara Mjini amesema eneo hilo kuna vumbi jingi sana lakini wahusika hawadhibitiwi na wananchi wanaendelea kuteseka.
Amesema NEMC imekuwa ikitoa matamko ambayo hayana mamlaka ya kuwawajibisha wanaosababisha vumbi hilo lakini watakapokuwa na mamlaka wanaamini wanaweza kuwadhibiti na kuacha kuchafua mazingira.
“Biashara ya makaa ya mawe ni changamoto kubwa hapa Mtwara hasa wakati wa upakiaji kwenye meli kuna magari hayajafunikwa yanasababisha vumbi kubwa sana hali ambayo inaathiri sana, NEMC ikiwa mamlaka itakuwa na uwezo wa kuwabana ili wafuate sheria,” amesema
“NEMC inakosa nguvu ya kuwawajibisha kisheria kama kuwatoza faini lakini ikiwa mamlaka usimamizi wa sheria ya mazingira itakua na tija, kuna gereji zinamwaga mafuta lakini wanashindwa kuwadhibiti kwasababu hawana nguvu yoyote,” amesema
“Kwa sasa NEMC ni baraza na haina uwezo wa kufanya maamuzi maamuzi mengi yanafaanywa na Wizara, NEMC wanaweza kufanya jambo Waziri akalitengua lakini wakiwa mamlaka watakuwa na nguvu ya kutenda bila maamuzi yao kutenguliwa kirahisi na waliojuu,” amesema