Kikwete aibuka, asema sijakufa, nipo salama

RAIS Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete amebainisha kuwa kitendo cha kuanika ukweli kuhusu maendeleo makubwa yaliyofanywa na Serikali chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, ndiyo yamewafanya baadhi ya watu kusema maneno ya ajabu, ikiwemo kudai kuwa yeye amekufa au anapaswa kupumzika.
Hata hivyo, Kikwete amebainisha hadharani kwamba hajafa, haugui popote na wala hajaamka na kichomi na kwamba wale wote wanaomuombea mabaya watakufa wao yeye ndio atakayeenda kuwazika. Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika mjini Bagamoyo, mkoani Pwani, Kikwete alisema baadhi ya watu wanadhani kwa sababu anazungumza kuhusu mafanikio makubwa ya CCM, basi labda amechoka kisiasa au amekufa jambo ambalo alisema si kweli hata kidogo.

“Mimi ninasema kwa haya maendeleo yanayoonekana chini ya CCM chama hiki kitaendelea kuchaguliwa, sasa nikiyasema haya kuna wengine wanasema huyu mzee apumzike wengine kafa. Nawaambia mimi mzima wa afya njema. Wanaosema nimekufa, watakufa wao na mimi nitaenda kuwazika,” alisema.
Alisema katika kipindi cha miaka minne na nusu ya uongozi wa Rais Samia, Tanzania imepiga hatua kubwa katika nyanja mbalimbali zikiwemo miundombinu, afya, elimu, nishati, utalii na uchumi kwa ujumla. SOMA: Tuache chokochoko tudumishe amani



