RAIS Mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete, amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa uamuzi wa kuunda kikosi kazi cha ukusanyaji wa maoni, kuhusu masuala ya siasa na kusema uwepo wake utasaidia kupunguza joto la kisiasa lililopo nchini.
Akizungumza muda mfupi baada ya kuwasilisha maoni yake, Kikwete amesema kuundwa kikosi kazi hicho ni kitendo cha kiungwana na busara zilizofanywa na Rais Samia, kuhakikisha demokrasia inazidi kukua nchini.
“Nimefurahi nimepata nafasi ya kuja mbele ya kikosi kazi hiki, itasaidia kupunguza joto ndani ya nchi, matumaini yake kitatusaidia kutengeneza maridhiano na mwenendo mzuri wa kufanya shughuli za kisiasa hapa nchini,” amesema Kikwete.
Kuhusu maoni aliyoyatoa mbele ya kikosi kazi hicho, Rais Kikwete amesema amejibu kutokana na namna ambavyo aliulizwa maswali, hivyo wao ndiyo wana jukumu la kuelezea kile alichowasilisha.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kikosi Kazi, Profesa Rwekaza Mukandala, amesema wamefarijika kupokea maoni ya Rais Kikwete na hasa kutokana na nafasi yake ya ufahamu katika masuala mbalimbali na wanaamini mchango wake utawasaidia kufikia lengo la jukumu walilopewa.
Amesema mbali na Rais Kikwete kikosi hicho pia kilipokea maoni kutoka kwa viongozi mbalimbali, taasisi na wadau wengine kwa njia ya mahojiano na maandishi na kesho watamaliza kupata maoni kutoka vyama vya siasa.
Amesema kwa sasa kikosi hicho kipo hatua za mwisho za kukusanya maoni yake, huku kikiendelea pia na kazi ya kuandaa ripoti na kwamba matarajio ifikapo mwishoni mwa wiki ijayo kazi hiyo rasmi itakuwa imekamilika.