‘Kuna ongezeko kubwa wagonjwa wa figo nchini’

DAR ES SALAAM : Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH)  imeadhimisha siku ya Figo Duniani inayofanyika Alhamisi ya pili ya mwezi Machi kila mwaka na kueleza uwepo wa ongezeko kubwa la wagonjwa wa figo nchini, wengi wao wakiwa na umri kuanzia miaka 40 hadi 50, huku wagonjwa 100 wakipandikizwa figo.

Akizungumza katika maadhimisho hayo jijni Dar es Salaam Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Muhimbili, Dk Delilah Kimambo amesema idadi ya wagonjwa wanaopata  huduma za kudumu za uchujaji wa figo nchini ni zaidi ya 3,000 na kwa hospitali hiyo ni zaidi ya wagonjwa 400.

“Watu wanaoishi mijini wanaathrika zaidi kwa asilimia 15 ikilinganishwa na wanaoishi vijijini kwa asilimia mbili na katika kipindi cha miaka 10 kuanzia mwaka 2015 na 2025 kumekuwa na ongezeko kubwa la wagonjwa wanaochuja damu kwa asilimia 203 na pia tumeshuhudia  ongezeko la sesheni za mizunguko ya uchujaji damu kwa asilimia 158 kutoka mizunguko 11,770  mwaka 2015 hadi sasa mizunguko 30,409 kwa mwaka 2025,” ameeleza.

Dk Kimambo amesema kutokana na ongezeko la ugonjwa huo na ongezeko la matibabu maalumu ya kupandikiza figo, hospitali ilianzisha huduma hiyo hadi sasa wagonjwa wapatao 100 wamepandikizwa figo katika hospitali hiyo tangu kuanza kwa huduma hiyo mwaka 2017.

“ Kwa huduma za nje za kliniki zetu za wagonjwa wa figo  zinahudumia wagonjwa wapatao 600 kila mwezi na kliniki  ya watoto takribani wagonjwa 120 kila mwezi,” amesema.

Amesema visababishi ni ugonjwa wa shinikizo la damu,kisukari, maambukizi ya VVU, matumizi holela ya dawa za maumivu na mitishamba, magonjwa ya saratani za njia ya mkojo mfano tezi dume na saratani ya mlango wa kizazi, magonjwa ya ndani ya figo,  uchafuzi wa hewa, joto kali, upungufu wa maji mwilini.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button