Latra yatangaza nauli mpya mwendo kasi, teksi

MAMLAKA ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (LATRA) imetangaza nauli mpya za teksi mtandaoni, pikipiki mtandao na Mabasi yaendayo Haraka (BRT) maarufu mwendokasi ambayo imepanda.

Nauli za mabasi ya mwendokasi kwa njia kuu kwa safari sasa ni Sh 750 kutoka Sh 650, njia mlisho Sh 500 kutoka Sh 400, njia mlisho ukijumlisha na njia kuu Sh 900 na njia ya Kimara kwenda Kibaha ni Sh 700.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari jana jijini hapa Mkurugenzi Mkuu wa Latra, Habibu Suluo alisema kiwango hicho kipya kitaanza kutumika baada ya siku 14.

Advertisement

Alisema kiwango cha nauli za teksi mtandao zenye uwezo wa kubeba abiria wasiozidi wanne nauli kiwango cha chini Sh 3,000 na kiwango cha juu ni Sh 4,000. Nauli ya kuanzia safari kiwango cha chini ni Sh 500 na kiwango cha juu ni Sh 1,000.

Nauli kwa kilometa kiwango cha chini ni Sh 800, kiwango cha juu Sh 1,000. Nauli kwa dakika ni Sh 80 na kiwango cha juu ni Sh 100. Ada ya kuita usafiri ni asilimia tatu.

Alisema kiwango cha kamisheni kiwango cha chini ni asilimia 10 na kiwango cha juu ni asilimia 20 na tozo ya Latra ni asilimia 0.5 na asilimia moja.

Alisema pikipiki mtandao zenye uwezo wa kubeba abiria wasiozidi wawili safari isiyozidi kilomita kiwango cha chini ni Sh 1,000 na kiwango cha juu ni Sh 1,500, nauli ya kuanza safari ni Sh 250 na kiwango cha juu ni Sh 350, nauli kwa kilomita ni Sh 300 na kiwango cha juu Sh 400.

Nauli kwa dakika ni Sh 500 na Sh 700, nauli kwa dakika ni Sh 50 na Sh 70.

Ada ya kuita usafiri ni asilimia mbili, kamisheni ni asilimia 10 na kiwango cha juu ni asilimia 20 tozo la Latra ni asilimia 0.5 na asilimia moja.

Pikipiki mtandao yenye uwezo wa kubeba abiria wasiozidi watatu safari isiyozidi kilomita ni Sh 2,000 na kiwango cha juu ni Sh 2,500, nauli ya kuanzia safari ni Sh 350 na Sh 500, nauli kwa kilomita ni Sh 500 na Sh 600, nauli kwa dakika ni Sh 70 na Sh 90, ada ya kuita usafiri ni asilimia 2.5, kamisheni ni asilimia 10 na asilimia 25 kwa nauli kiwango cha juu na Latra ni asilimia 0.5 na asilimia moja.

Alisema nauli za teksi mtandao na pikipiki mtandao ni suala ambalo liliwatoa baadhi ya watoa huduma lakini sasa marekebisho yamefanyika wana hiari ya kuendelea kutoa huduma au la.

Alisema kuwa baadhi ya maoni yaliyopokelewa ni mapendekezo ya nauli kutoka Kimara hadi Kibaha iwe Sh 1,200 lakini baada ya bodi kukaa iliamua nauli isizidi Sh 700.

Mapendekezo mengine ilikuwa kutaka nauli kwa wanafunzi iwe Sh 300 badala ya Sh 200 ambapo alisema “Tuliamua nauli iendelee kubaki Sh 200 kwa wanafunzi.”