Lissu: Tusameheane tuijenge Chadema

Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu.

MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu amesihi wanachama wa chama hicho wasameheane.

Lissu amesema hayo Dar es Salaam wakati wa hafla ya kukabidhiwa ofisi katika makao makuu ya chama hicho.

“Uchaguzi uliotufanya tusemezane vibaya umepita, sababu iliyotufanya tuvutane imepita na imepita kwa namna ambayo nchi hii nzima inaisifia, kwa hiyo kwa sababu tumefanya jambo ambalo kila mtu amelisifia, bado tuna sababu ya kuendelea kuvutana? bado tuna sababu ya kuendelea kusemana vibaya? bado tuna sababu ya kunyosheana vidole machoni? hapana, tunarudi wote nyumbani, kwa sababu wote ni wa nyumba moja,” alisema.

Advertisement

Ameongeza: “Baada ya kelele zote hizi turudi nyumbani, tuendelee kujenga palipo bomoka, palipo pasuka tupazibe, palipo haribika tuparekebishe wote.”

Lissu amesema safu ya uongozi iliyochaguliwa ni viongozi wanaopenda mabadiliko na watahakikisha wanakiletea mabadiliko chama hicho.

“Kwa hiyo ni lazima kuwe na mabadiliko ya ndani ya chama ambayo nitaomba tuyafanye pamoja na ya nje ya chama, nitaomba tuyapiganie pamoja kwa sababu tunahitaji mabadiliko ndani ya chama na mabadiliko katika nchi hata ya
ndani,” amesema.

Ameongeza: “Yanatuhusu, haki mnajua inainua Taifa na haki inainua chama kwa hiyo hatutaonea mtu, hatutakubali mwanachama yeyote aonewe kwa hiyo tegemeeni mabadiliko kwa haki.”

Lissu amesema hatochagua mwanachama atakayeongoza nafasi yeyote kwenye uongozi wa chama hicho kwa kumuonea mwanachama mwenye haki.

“Kama kuna mtu anafikiria kwamba atapata isiyokuwa haki yake kwa sababu yeyote ile, ninapendekeza kwake akafikirie tena, kuna vitu vingi na kazi kubwa ya kufanya. Tutahakikisha tunaifanya kwa pamoja na tunaifanya kwa
haki,” amesema.

Lissu alitoa wito kwa wanachama wengine kujiunga na chama hicho na wadau wajitokeze kukisaidia chama hicho kwa misaada mbalimbali.

“Ninapenda kuwakaribisha wananchi kujiunga na chama hiki ili kuongeza nguvu ya mapambano na ninatumia nafasi hii kuwaomba wadau kutusaidia misaada mbalimbali, mwenye maji ya kunywa tunapokea, mafuta ya
magari tunapokea na fedha ili kutuwezesha kufanya mapambano haya vizuri,”amesema.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *