Mabasi mapya 177 ya mwendokasi kuinogesha Dar

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Innocent Bashungwa amesema serikali ipo  hatua za mwisho za kusaini mkataba wa kununuliwa mabasi mapya 177 ya mwendokasi ya Wakala wa Usafiri wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) jijini Dar es Salaam.

Bashungwa ameeleza hayo leo Septemba 3, 2022  alipoambatana na Kamati ya Kudumu ta Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC), kutembelea na kukagua miradi ya Wakala wa Usafiri wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) Dar es Salaam.

Bashungwa ameeleza ogezeko la mabasi hayo litawezesha DART kuongeza huduma kwa wananchi kutoka kuhudumia abiria 200,000 hadi kufikia 500,000 kwa siku vituo vyote vilivyopo sasa Dar es Salaam.

Advertisement

“Mabasi ya mwendokasi yamepunguza kwa asilimia kubwa msongamano wa magari Mkoa wa Dar es Salaam na kuwawezesha wananchi kutumia muda mwingi kwenye kufanya kazi za uzalishaji, pia kuwawezesha wanafunzi kufika shuleni mapema bila adha kubwa za foleni,” amesema Bashungwa.

Waziri bashungwa pia amemuagiza Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI, Prof. Riziki Shemdoe kusimamia kikamilifu DART kufanya usanifu kwa haraka katika maeneo ambayo yapo pembezoni, ili kuweka mpango wa kufikisha huduma ya mabasi ya mwendokasi, kama maeneo ya Vikindu, Kigambo, Ukonga  na Chanika.

Amesema dhamira ya serikali ni kuongeza mtandao wa barabara za mwendokasi, kwa kufikisha huduma ya mabasi katika maeneo pembezoni yenye watu wengi na kuboresha huduma katika maeneo ambayo yana huduma za mabasi ya mwendokasi.

Naye, Mwenyekiti wa Kamati PIC, Jerry Silaa amepongeza DART  kwa kutumia mifumo ya TEHAMA katika utoaji huduma na kuwezesha mapato kuongezeka kutoka Sh bilioni 25 hadi Sh bilioni 36 kwa mwaka wa fedha 2021/22.

/* */