Madini wakusanya zaidi ya bil 902/-

WAZIRI wa Madini, Anthony Mavunde, amebainisha kuwa Sekta ya Madini nchini imeendelea kupiga hatua kubwa, ambapo maduhuli ya zaidi ya shs bilioni 902 sawa na asilimia 90.2 ya lengo la kukusanya Shs trilioni moja kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 kufikia Mei 15, 2025.

Hatua hiyo ni kabla ya kumalizika kwa Mwaka wa Fedha, huku zikiwa zimesalia zaidi ya siku 45, jambo linalotoa matumaini makubwa kuwa lengo litafikiwa kwa asilimia 100.

SOMA: Serikali yavuna bil 183/-masoko ya madini

Mavunde ameyasema hayo leo Mei 15 alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma kuhusu mafanikio makubwa yaliyopatikana katika Kipindi cha Miaka Minne ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.

Waziri Mavunde ameeleza kuwa, Sera ya Madini ya Mwaka 2009 na Mpango wa Miaka Mitano wa Maendeleo ya Taifa ulielekeza Sekta ya Madini ikichangia asilimia 10 ya Pato la Taifa ifikapo mwaka 2025.

Hata hivyo, tayari mwaka 2024 sekta hiyo imefikia mchango wa asilimia 10.1, ikiwa ni mafanikio yaliyotangulia muda uliopangwa.

“Tumefanikiwa kuvuka lengo la kitaifa. Mwaka 2021 Sekta ya Madini ilichangia asilimia 7.3 kwenye pato la Taifa, mwaka 2023 ilifika asilimia 9.1, na hivi sasa tupo kwenye asilimia 10.1 kufikia mwaka 2024. Hili ni jambo la kujivunia,” amesema Mavunde.

Katika kipindi hicho, maduhuli ya Serikali kupitia Sekta ya Madini yameongezeka kwa zaidi ya asilimia 20, kutoka Shs bilioni 623.24 mwaka 2021/2022 hadi kufikia bilioni 753.18 mwaka 2023/2024.

Amesema hadi kufikia Mei 9, 2025, Wizara ya Madini ilikuwa imekusanya Shilingi bilioni 902, sawa na asilimia 90.2 ya lengo la mwaka.

Waziri Mavunde amesema Sekta ya Madini imeendelea kuwa mhimili mkubwa wa upatikanaji wa fedha za kigeni.

Mnamo mwaka 2023, mauzo ya madini nje ya nchi yalifikia Dola za Marekani bilioni 3.55, yakichangia asilimia 46.1 ya mauzo yote ya bidhaa nje ya nchi.

Aidha, kampuni za wazawa zimenufaika kwa kiasi kikubwa.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button