MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam imemwachia huru, Omary Hassan maarufu kama Mbegu aliyekuwa anakabiliwa na shitaka la kumuua kwa kukusudia Mwasiti Yasin aliyekuwa mhasibu wa Kampuni ya Grants Care Limited, baada ya ushahidi wa upande wa mashitaka kushindwa kuthibitisha shitaka dhidi yake.
Akisoma hukumu hiyo jana, Hakimu Mkazi Mkuu, Renatus Rutta alisema wakati wa usikilizwaji wa shauri hilo upande wa mashitaka walipeleka mashahidi wanane.
Hakimu Rutta alisema katika ushahidi uliotolewa na mashahidi hao, hakuna sehemu ambapo mshitakiwa ameguswa moja kwa moja, hivyo alimwachia huru.
“Katika mashahidi ambao waliletwa na upande wa mashitaka kutoa ushahidi dhidi yake, hakuna ushahidi ambao umeweza kumgusa mshitakiwa, ninamwachia mshitakiwa huru,” alisema Hakimu Rutta.
Kwa mujibu wa hati inadaiwa kuwa katika eneo la Uhuru na Sikukuu, Omary Hassan maarufu kama Mbegu alimuua kwa kumshambulia kwa risasi Mwasiti Yasin.
Inadaiwa marehemu akiwa ni Mhasibu wa Kampuni ya Grants Care iliyoko eneo la Kariakoo, Dar es Salaam, akiwa njiani mtaa wa Uhuru /Swahili kuelekea katika benki ya Habibu Afrika akiwa na Sh milioni 7.2 alivamiwa na majambazi kisha walimpiga risasi nakuchukua fedha hizo.