DAR-ES-SALAAM: Mahmoud Thabit Kombo ni kiongozi maarufu ambaye amechangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya biashara na siasa nchini Tanzania. Kuanzia miaka ya mapema ya 1990, Kombo amekuwa akiongoza katika nyanja mbalimbali, na kuweka alama ya mafanikio.
Kombo alianza safari yake ya kitaaluma mnamo mwaka 1996/1998 alipokuwa Meneja wa Biashara katika Kampuni ya Datel Tz Limited. Baada ya hapo, kati ya 1998 na 1999, alihamia kuwa Meneja wa Uendeshaji katika Kampuni ya Komyuta Micronix.
Kuanzia mwaka 1999 hadi 2001, alihamishia ujuzi wake katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, akiwa Afisa Mkuu wa Mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano katika Idara ya Kazi. Katika kipindi cha mwaka 2001 hadi 2004, alihudumu kama Meneja wa Uendeshaji na Msimamizi Mkuu wa Biashara katika Kampuni ya Zantel, ambapo alijizolea uzoefu muhimu katika sekta ya mawasiliano.
Katika medani za siasa,Kombo alijitosa rasmi mwaka 2005 akiwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi (NEC) Taifa, nafasi aliyoshikilia hadi mwaka 2010. Aliendelea kufanya kazi katika nafasi nyingine muhimu ndani ya Chama cha Mapinduzi, ikiwa ni pamoja na Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Wilaya na Mkoa. Mwaka 2012 hadi 2017, alihudumu kama Mweka Hazina wa Wilaya wa Chama cha Mapinduzi na pia alishiriki katika kamati za kampeni za uchaguzi za Tanzania Bara na Visiwani mwaka 2015/2016.
Kombo alikamilisha masomo yake katika Chuo Kikuu cha Sunderland nchini Uingereza, akipata shahada ya uhasibu na masuala ya kompyuta. Aliendeleza elimu yake kwa kufanya masomo ya uzamili katika Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT) na AI, pamoja na masuala ya kimataifa na diplomasia.
Kufuatia mafanikio yake ya kipekee na uzoefu wa kimataifa, mwaka 2023 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alimteua Mahmoud Thabit Kombo kuwa Balozi wa Tanzania nchini Italy. Hivi karibuni, ameteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kanda ya Afrika Mashariki.
SOMA: Chuo cha DMI kuja kivingine
Mahmoud Thabit Kombo anaendelea kuchangia kwa kiasi kikubwa katika maendeleo ya Tanzania, akionyesha uongozi thabiti na maono ya kisasa katika nyanja za biashara, siasa, na diplomasia.