ZANZIBAR; SERIKALI imeonya wanaoidhikaki serikali na viongozi mitandaoni.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni alionya pia watu wasithubutu kuchezea amani na akasema italindwa kwa gharama yoyote.
Masauni alitoa onyo hilo Zanzibar jana wakati akifungua mafunzo ya uongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na jumuiya zake.
Aliagiza viongozi katika maeneo yao wafikishe ujumbe kwa kusema mazuri na mafanikio yaliyopatikana ili wapinzani wasipate mwanya wa kuficha mazuri yaliyopatikana.
Isome:https://habarileo.co.tz/kinana-aonya-wanaomtusi-rais-samia/
Masauni alimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi kwa kuwa licha ya propaganda za wapinzani hawajatetereka.
‘Sisi tuwe mfano wa kufuata nyayo zao, wapo watu waliona kwamba kwa sababu hakuna ajenda, ilani imetekelezwa kwa kiwango kikubwa kabla hata ya wakati, hawa wapinzani wakaona labda pengine watafanya vipi kuteteresha umoja na mshikamano uliopo,”alisema.
Masauni alipongeza busara za Rais Samia na Dk Mwinyi kwa kuwa wametulia na wanafanya mambo kwa vitendo na hawajatoka kwenye reli.
“Haya yanayofanywa si tu kutaka kututoa kwenye reli. Dhamana nimepewa mimi, mimi ndiye Waziri wa Mambo ya Ndani ninayesimamia polisi na vyombo vya usalama, watu watafanya uchaguzi katika nchi hii kwa usalama na amani na mtu yeyote asijaribu kucheza na amani ya nchi hii, hilo ni jambo la msingi, tutailinda amani na usalama wa nchi hii kwa gharama yoyote”.