Mbio zahamasisha ujenzi uwanja Muhas

MKURUGENZI wa Kinga kutoka Wizara ya Afya, Dk. Ntuli Kapologwe amesema mbio za ‘Reunion Fun Run’ zilizoandaliwa kwa msimu wa tatu na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) zimelenga kutengeneza miundombinu ya michezo ya chuo hicho, sambamba kujikinga na magonjwa mbalimbali.

Mbio hizo zinakutanisha wahitimu mbalimbali wa Muhas na familia zao kwa ajili ya kuhamasisha mazoezi kwa jamii.

Advertisement

Akizungumza leo Novemba 23, 2024 mara baada ya kukamilisha mbio hizo za kilomita 5, 10 na 15 chuoni hapo. Dk Kapologwe amesema hatua hiyo inalenga pia kutekeleza kampeni ya kitaifa ya Mtu ni Afya katika kujikinga na magonjwa mbalimbali.

“Mbio pia zinalenga kuhamasisha kampeni Mtu ni Afya, chini ya kampeni Fanya Kweli Usibaki Nyuma,” amesema Dk Kapologwe.

Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Muhas, Prof. Appolinary Kamuhabwa amesema mbio hizo ni maalum kwa ajili ya kuhamasisha ujenzi wa uwanja wa michezo kwa kutafuta rasilimali fedha zitakazofanikisha suala hilo.

Amesema upataikanaji wa uwanja huo utabadilisha maisha ya watumishi na wanafunzi kwenye suala la michezo kwa kulinda afya zao.

“Kutakuwa na uwanja wa basketi, netiboli, mpira wa miguu, gym ndogo, ni kituo ambacho kitaendana na majukumu yao,” amesema Prof Kamuhabwa.

Aidha amesema kuwa mahitaji ya  fedha ya kukamilisha zoezi hilo ni makubwa , hivyo ameitaka jamii, wakiwemo wadau wa michezo kuchangia zoezi hilo ili kufanikisha suala hilo.

Akitoa historia fupi wakati akizungumza na HabariLeo, Rais wa Muhas, Marsha Macatta-Yambi amesema kipindi cha nyuma uwanja uliopo kwa saa ulikuwa mdogo tofauti ulivyo kwa sasa, hivyo ujenzi wa uwanja miundombinu mipya ya michezo itasaidia kuimarisha afya.

“Kwahiyo hatua hii itasaidia kuendana na changamoto ya magonjwa nyemelezi,” amesema Marsha Macatta-Yambi , na kuongeza kuwa: “Pia itasaidia jinsi ya kuweka alama kuwatambua wanaoweka mikono yao katika zoezi hili.”

Pendo Paul, mwanafunzi wa mwaka wa kwanza Shahada ya Uuguzi Muhas ameiomba jamii kuhakikisha inakuwa na tabia ya kufanya mazoezi ili kulinda afya zao.