PARIS: Mcheza tenisi namba 1 duniani kwa mchezaji mmoja mmoja anayetambuliwa na chama cha wachezaji wa kulipwa Jannik Sinner amejiondoa kwenye Michezo ya Olimpiki ilitakayofunguliwa jijini Paris, Ufaransa Julai 26 baada ya kuugua uvimbe wa tonsili.
Hivi karibuni nyota huyo wa kitaliano alihisi kizunguzungu na kutoka nje ya uwanja wa tenisi wakati wa mchezo wa robo fainali wa michuano ya Wimbledon aliposhindwa na Daniil Medvedev mapema mwezi huu.
Sasa Sinner, 22, amelazimika kukosa michezo ijayo jijini Paris na amethibitisha habari hizo kupitia mtandao wake wa kijamii.
SOMA: Collins, Sophia waitaka rekodi Olimpiki
Katika mtandao wa X, Sinner ameandika: “Nahuzunishwa kuwajulisha kuwa kwa bahati mbaya zitaweza kushiriki katika Michezo ya Olimpiki ya Paris.”

Amesema baada ya wiki ya mazoezi alianza kujihisi vibaya hivyo kutumia siku kadhaa kupumzika na alipokwenda kwa daktari aligundulika kuwa na tonsili aliyemshauri kutocheza.
“Kukosa michezo ni jambo la kuvunja moyo sana kwani ilikuwa moja ya malengo yangu makuu kwa msimu huu. Nilikuwa na hamu kubwa ya kupata heshima ya kuiwakilisha nchi yangu katika tukio hili muhimu sana,”amesema Sinner.
Michezo ya tenisi itafanyika kuanzia Julai 27 hadi Agosti 4.
Sinner amekuwa mmoja wa nyota tenisi kwa mchezaji ja mmoja waliotarajiwa kutwaa medali ya dhahabu katika Michezo ya Olimpiki lakini kufuatia kujitoa sasa Novak Djokovic anatarajiwa kuwa mchezaji namba moja.

Tanzania itawakilishwa na wanamichezo 15 katika michezo mwaka huu ukiwemo mchezo wa kuogelea.
Olimpiki ni matukio ya michezo ya kimataifa inayojumuisha mashindano ya majira ya baridi na kiangazi ambapo aelfu ya wanamichezo kutoka maeneo mbalimbali duniani hushiriki michezo mbalimbali.
Michezo ya Olimpiki inachukuliwa kuwa mashindano makubwa zaidi ya michezo duniani, ikiwa na zaidi ya timu 200, zinazowakilisha nchi huru na maeneo, zinazoshiriki.
Michezo ya Olimpiki ya Paris 2024 itahudhuriwa na wanamichezo kutoka nchi 206. Michezo hiyo hufanyika kila baada ya miaka minne.
Marekani itakuwa na idadi kubwa zaidi ya wanamichezo wanaoshiriki Michezo ya Olimpiki ya Paris 2024, ikiwa na ujumbe wa wanamichezo 653.
Nchi mwenyeji, Ufaransa, inafuatia kwa karibu na wanamichezo 622, na Japan ikiwa na wanamichezo 447