Mgodi wa Magambazi kuanza kazi Julai

WAZIRI wa Madini, Anthony Mavunde, ameeleza kuwa Mgodi wa Kati wa Dhahabu wa Magambazi uliopo Wilayani Handeni Mkoa wa Tanga utaanza kufanya kazi rasmi ifikapo Julai 2025 na unatarajiwa kuleta tija kwa kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika Kijiji cha Nyasa na Wilaya ya Handeni kwa ujumla.
Waziri Mavunde ameeleza hayo leo Mei 10 wakati akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Nyasa, Kata ya Kang’ata, Wilaya ya Handeni, alipokwenda kupeleka mrejesho wa ahadi aliyotoa Aprili 6, kuhusu hatma ya uendelezaji wa mgodi huo uliosubiriwa kwa muda mrefu.
“Tunamshukuru sana Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maelekezo yake kuhakikisha Mgodi huu wa Magambazi unaanza kufanya kazi na kuwainua wananchi wa hapa na mnyororo mzima wa shughuli za maendeleo,” amesema Mavunde.

Amesema baada ya kuchukua hatua ya kupata muafaka wa kuhakikisha mgodi huo unaanza kufanya kazi, kampuni nyingine ya tatu itateuliwa ndani ya siku 14 kati ya Mei 12 na 26, ambayo itaungana na Kampuni za PMM na East African Metals/CANACO ili kuendesha mgodi huo.
Waziri Mavunde amesema: “Kipekee nawashukuru sana wananchi wa Nyasa kwa uvumilivu wenu, hili jambo lilikuwa la muda mrefu tangu tumeanza kulifanyia kazi, mlikubali kukaa hapa na kunyeshewa na mvua, na leo mmekuja tena na kukubali kukaa nami kwenye mvua ili kuwapa mrejesho wenu.”

Ameziagiza kampuni zinazoendesha mgodi huo kuhakikisha zinatoa kipaumbele kwa wakazi wa Nyasa katika ajira ili wananchi wanufaike moja kwa moja na uwepo wa mgodi katika Kijiji chao.
Azmezitaja faida zitakazopatikana kuwa ni pamoja na kuinua mapato ya Halmashauri ya Wilaya ya Handeni, uboreshaji wa miundombinu ya afya, elimu, barabara na mengine kupitia Wajibu wa Kampuni kwa Jamii (CSR) pamoja na ushiriki wa Watanzania katika mgodi huo kwa kutoa huduma na kuuza bidhaa (Local Content).