Michuano ya kuogelea yaanza leo Dar

DAR ES SALAAM: Michuano ya kuogelea ya Klabu Bingwa Taifa imeanza leo kwenye bwawa la kuogelea la Shule ya Kimataifa ya Tanganyika (IST) na kushirikisha wachezaji vijana 112 kutoka klabu mbalimbali.
Tayari wachezaji wawili walioanza mapema asubuhi wamevunja rekodi ya kitaifa ingawa bado wanaendelea kuangalia wengine mpaka kufika kesho itajulikana idadi kama imeongezeka.
Akizungumza na HabariLEO, Mwenyekiti wa Chama cha Kuogelea Tanzania (TSA), David Mwasyoge amesema kitendo cha wachezaji kuvunja rekodi mapema inaonesha ushindani na juhudi za klabu na makocha katika kuwanoa wachezaji wao.
“Mpaka sasa hivi (muda wa saa tatu asubuhi) kuna rekodi mbili zimeshavunjwa na tunaendelea mpaka jioni watafika wangapi. Tunaendelea mpaka kesho wanaweza kuongezeka,” amesema Mwasyoge ambaye aliongeza kuwa wachezaji wote waliovunja rekodi watatajwa baadaye.
Amesema kufanya huko vizuri kwa wachezaji kunawapa matumaini kwani msimu huu wataangalia zaidi viwango vya wachezaji.
Washindi watapewa medali na zawadi mbalimbali zilizoandaliwa kwa ajili ya kuwapa motisha wachezaji kuongeza bidii.