Mikopo 10% yaiva, mfumo, kanuni tayari

DAR ES SALAAM;  MAANDALIZI ya kanuni na mwongozo kwa ajili ya kutoa mikopo ya asilimia 10 katika halmashauri kwa ajili ya wanawake, vijana na wenye ulemavu yamekamilika, imefahamika.

Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kupitia ukurasa wake katika mtandao wa kijamii wa X, imeeleza kuwa Katibu Mkuu Tamisemi, Adolf Ndunguru alibainisha hayo Dodoma wakati anafungua mafunzo ya mikopo ya asilimia 10 kwa wawezeshaji wa kitaifa.

Katibu Mkuu Ndunguru ameagiza wawezeshaji hao watumie mafunzo watakayoyapata ili malengo ya kutoa mikopo hiyo yatimie kwa kuwa Rais Samia Suluhu Hassan ameagiza irudishwe na isimamiwe vizuri.

“Ninafahamu kuwa uandaaji wa kanuni, mwongozo, vitini vya mafunzo pamoja na maboresho ya mfumo wa kielektroniki wa utoaji na usimamizi wa mikopo kwa vikundi umekamilika,” alisema Ndunguru.

“Niwapongeze wote mlioshiriki kukamilisha nyenzo zitakazowezesha utoaji wa mafunzo kwa wasimamizi na vikundi kabla ya kuanza kutoa mikopo kama ilivyoelekezwa na serikali,” aliongeza Ndunguru.

Soma pia:https://habarileo.co.tz/kairuki-apokea-mapendekezo-mikopo-ya-10/

Mkurugenzi wa Tawala za Mikoa, Ofisi ya Rais Tamisemi, Beatrice Kimoleta alisema wamefanya masuala mbalimbali kuboresha mikopo hiyo kwa kufanya marekebisho ya Sheria ya Fedha, mapitio ya kanuni za mikopo, uandaaji wa miongozo na vitini vya mafunzo.

Kimoleta alisema baada ya mafunzo hayo, wawezeshaji 840 watajengewa uwezo na baada ya hapo watatoa mafunzo kwa kamati za uratibu wa mikopo ngazi ya mikoa, halmashauri na kata kuhusu nafasi zao katika kusimamia utoaji wa mikopo ya vikundi.

Wakati akiwasilisha bungeni Dodoma makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2024/25, Waziri wa Tamisemi, Mohamed Mchengerwa alisema serikali inarejesha mikopo ya asilimia 10 kupitia halmashauri kuanzia Julai mwaka huu.

Mchengerwa alisema Tamisemi imesanifu na kujenga mfumo wa Wezesha Portal utakaotumika kutoa mikopo hiyo.

Alisema mfumo huo utasaidia kuondoa changamoto za awali ikiwamo kuondoa vikundi hewa, watu kujisajili zaidi ya kikundi kimoja na wakopaji hewa.

Aidha, alisema mfumo huo utaimarisha usimamizi, usajili wa vikundi, utoaji na urejeshaji wa mikopo hiyo na upatikanaji wa taarifa sahihi za mikopo kwa wakati ili kuongeza tija, kuondoa upendeleo na kuongeza uwazi na uwajibikaji.

Mchengerwa alisema mambo kadhaa yatafanyika ikiwamo kuanzisha kitengo cha usimamizi wa mikopo ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu katika Ofisi ya Rais –Tamisemi na uanzishwaji wa kamati za usimamizi wa mikopo katika ngazi za ofisi za wakuu wa mikoa, halmashauri na kata.

Majukumu ya kamati ngazi ya kata ni kutambua waombaji na kuthibitisha vikundi vya mikopo na kuvisajili kwenye mfumo kabla ya kuwasilisha kwenye kamati ya halmashauri.

Alitaja maboresho mengine ni kujenga uwezo kwa wasimamizi wa mikopo hiyo kwa kuongeza idadi ya wasimamizi wa mikopo kwenye ngazi ya kata na maofisa maendeleo ya jamii 787 wameajiriwa na kupangiwa kata zilizokuwa na upungufu.

Mchengerwa alisema mikopo inayotarajiwa kutolewa ni Sh bilioni 227.96 zikiwamo Sh bilioni 63.67 za marejesho zilizokuwa zikiendelea kukusanywa kutokana na mikopo iliyotolewa kabla ya kusimamishwa.

“Shilingi bilioni 63.24 ni fedha zilizokuwa zinatengwa kwa ajili ya mikopo na shilingi bilioni 101.05 ni fedha ambazo zimetengwa kutokana na makisio ya makusanyo ya mapato ya ndani ya mwaka 2024/25,” alifafanua Mchengerwa.

Habari Zifananazo

Back to top button