Mlipuko wa bomu waua watu 26 Pakistan

Wachunguzi wakikusanya ushahidi kutoka kwenye eneo la mlipuko wa bomu kwenye kituo cha treni katika mji wa Quetta, Pakistan(Picha na AP)

WATU 26 wamekufa na wengine wapatao 62 kujeruhiwa baadhi vibaya baada ya mtu aliyejitoa muhanga kujilipua kwa bomu leo kwenye kituo cha treni Kusini Magharibi mwa Pakistan.

Msimamizi wa usalama kwenye kituo cha treni katika mji wa Quetta, Shahid Nawaz amesema mshambuliaji alijifanya abiria na kujilipua miongoni mwa abiria waliokuwa wakisubiri treni kwenda mji wa Rawalpindi.

SOMA: Taliban yakana kushambulia msafara

Advertisement

Baadhi ya waathirika wa mlipuko walipelekwa hospitali ya serikali na wengine kwenye hospitali ya jeshi.

Miongoni mwa waliokufa ni pamoja na wanajeshi na wafanyakazi wa reli.

Katika taarifa kundi linalotaka kujitenga la Balochistan Liberation Army, limedai kuhusika na shambulio hilo likisema mlipuaji wa bomu alilenga wanajeshi waliokuwa kwenye kituo cha treni.