Mloganzila kurekebisha mishipa ya kuchuja damu

DAR ES SALAAM: HOSPITALI ya Taifa Muhimbili–Mloganzila imeandaa kambi maalumu ya kutengeneza na kurekebisha mishipa ya kuchuja damu kwa wagonjwa wenye changamoto za figo kwa lengo la kuboresha upatikanaji wa huduma bora na salama za kuchuja damu.
Kambi hiyo maalumu inatarajiwa kuanza Februari 14 hadi 18, 2026 jijini Dar es Salaam.
Akizungumza kuhusu kambi hiyo, Daktari Bingwa wa Upasuaji, Dk David Antanamsu amesema kambi itahusisha wataalam bingwa wa ndani, ambapo wagonjwa ambao bado hawajawekewa mishipa ya kuchuja damu pamoja na wale waliowekewa kwa muda mrefu lakini mishipa hiyo imeshindwa kufanya kazi, watanufaika na huduma hiyo.
Dk Antanamsu amebainisha kuwa utengenezaji wa mishipa ya kuchuja damu una faida nyingi ikiwemo kupunguza hatari ya maambukizi, kuongeza muda wa matumizi ya mshipa huo, pamoja na kupunguza gharama za kubadilisha mpira (catheter) mara kwa mara, hali inayochangia kuboresha afya na ubora wa maisha ya wagonjwa.
Kwa kuandaa kambi hiyo Mloganzila inaendelea kuimarisha utoaji wa huduma za ubingwa na ubingwa bobezi hapa nchini, kuanzisha huduma bunifu zenye tija kwa jamii, na kuunga mkono jitihada za Serikali za kusogeza huduma za afya karibu na wananchi huku ikisisitiza ubora, usalama na ufanisi wa huduma zinazotolewa.



