DAR ES SALAAM – Aliyekuwa Mwanasiasa wa upinzani nchini, Mchungaji Peter Msigwa amefunguka mazito mara baada ya kupokelewa na Chama cha Mapinduzi (CCM) akidai ameondoka CHADEMA kwa sababu ya ubinafsi wa Mwenyekiti wa chama hicho Freeman Mbowe.
Msigwa amemtuhumu Mwenyikiti wa Chadema kuwa ameshindwa kuruhusu wajumbe wengine kuongoza chama hicho wala kugombe katika nafasi kubwa, Urais. Msigwa amesema “(Mbowe) amekigeuza chama kama SACCOS. Chama ni Taasisi.”
Mwanasiasa huyo ambaye pia alikuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema alitambulishwa CCM, Dar es Salaam jana wakati wa kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Taifa iliyoongozwa na Mwenyekiti wa CCM, Rais Samia Suluhu Hassan.
Msigwa amewahi kuwa Mbunge wa Iringa Mjini kupitia Chadema kuanzia mwaka 2010 hadi 2020. Wakati Msigwa anakwenda kutambulishwa kwa wajumbe wa NEC viongozi hao walikuwa wakiimba wimbo wa ‘tuna imani na Samia, tuna imani na CCM’.
SOMA: Majaliwa ataka mpango kuwezesha waraibu
Msigwa alikwenda mbele ya wajumbe wa NEC ya CCM akiwa ameongoza na Katibu Mkuu wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi na alishikwa mkono aende kumsalimia Rais Samia, Makamu wa Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi na Makamu Mwenyekiti wa CCM bara, Abdulrahman Kinana.
Baada ya Msigwa kuwasalimia viongozi wa meza kuu wakati anaondoka wajumbe wa NEC walikuwa wakiimba “Mlete Msigwa, mlete Msigwa, mlete Msigwa” Naye Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Godbless Lema kupitia ukurasa wake katika mtandao wa kijamii wa X aliandika kuwa uamuzi wa Msigwa umemuumiza sana.
“Ningetamani kuendelea kufanya kazi na wewe katika chama bora Chadema,” aliandika Lema. Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi(UVCCM), Mohammed Kawaida kupitia ukurasa wake wa X alimpongeza Msigwa kwa kuhamia CCM na akawakaribisha na wengine.
View this post on Instagram
“Karibu sana kwenye chama cha kutenda haki na chenye kusimamia vyema ajenda za Taifa letu la Tanzania Mchungaji @ MsigwaPeter, ”aliandika Kawaida. Katika uchaguzi wa Chadema, Kanda ya Nyasa Mei 29, mwaka huu Msigwa alishindwa kutetea nafasi ya uenyekiti wa kanda hiyo baada ya kuzidiwa kwa kura mbili na Mbunge wa zamani wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi (Sugu) .
Mbilinyi alipata kura 54, Msigwa alipata kura 52, alidai kuhujumiwa alitangaza kukata rufaa. Juni 3, mwaka huu alipozungumza na waandishi wa habari mkoani Iringa alidai kuwa ushindi aliopata Mbilinyi haukuwa halali. Alidai kuwa mifumo ya chama imetumika kumhujumu ili asishinde na kuwa kulikuwa na mbinu chafu dhidi yake ili asishinde.
Aidha, Juni 3, mwaka huu Katibu wa NEC ya CCM Itikadi, Uenezi na Mafunzo , Amos Makalla akiwa katika mkutano wa hadhara Arusha Mjini wakati wa ziara ya Dk Nchimbi alimkaribisha Msigwa katika chama hicho.