Msigwa kunguruma Iringa Ijumaa

IRINGA; CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Iringa Mjini kimempokea mwanachama wake mpya kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Peter Msigwa ofisini kwao mjini hapa.

Mkutano mkubwa wa hadhara wa kumkaribisha utafanyika keshokutwa Ijumaa katika Viwanja vya Mwembetogwa.

Akiwa katika ofisi hizo, Msigwa alisaini vitabu vya chama hicho na Katibu wa CCM Iringa Mjini, Hassan Makoba na wajumbe wa Kamati ya Siasa ya wilaya hiyo walionesha furaha.

“Tunafurahi sana kumkaribisha mtu mashuhuri kutoka chama kikuu cha upinzani katika familia yetu. Hatua hii inaashiria dhamira yetu ya umoja na maendeleo kwa taifa letu,” alisema Makoba.

Hivi karibuni, wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM walimkaribisha Msigwa katika chama hicho tawala wakiongozwa na Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Samia Suluhu Hassan.

“Nimekuja hapa kupata taratibu, kanuni na miongozo mingine ya chama kuelekea ujenzi zaidi wa chama chetu CCM, mambo mengine mengi nitazungumza kwa ufasaha sana katika mkutano wetu wa hadhara utakaofanyika Ijumaa Julai 12,” alisema Msigwa jana.

Alisema katika mkutano huo atatoa sababu kwa nini Dk Samia na CCM wanapaswa kuaminiwa tena.

Isome pia: https://habarileo.co.tz/msigwa-afunguka-mazito-akihamia-ccm/

Msigwa aliyewahi pia kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema Taifa na Mwenyekiti wa Kanda ya Nyasa, kuhamia CCM inaonekana kama pigo kubwa kwa Chadema Iringa Mjini ambayo imekuwa moja ya ngome zake kubwa katika ulingo wa siasa kwa miaka mingi.

Meya wa Manispaa ya Iringa, Ibrahim Ngwada ameelezea matumaini kwamba ushirikiano huo mpya utaimarisha nafasi yao na kuleta mitazamo mipya na kuchochea mikakati yao katika kufanikisha Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka huu na Uchaguzi Mkuu wa mwakani.

“Tunayo furaha kubwa kukukaribisha katika familia yetu. Tunajivunia kuwa na wewe na tunatarajia ushirikiano mzuri na mafanikio makubwa ya pamoja. Karibu sana, tuungane kwa pamoja katika safari hii ya kujenga taifa letu kwa umoja na nguvu mpya,” alisema Ngwada.

Habari Zifananazo

Back to top button