Msuya asimulia makubwa ya Nyerere kabla hajafa (2)

JANA makala hii inayotokana na mahojiano maaalumu ya Septemba 2016 baina ya vyombo vya habari vya Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN), likiwamo gazeti la HabariLEO na Makamu wa Kwanza wa Rais na Waziri Mkuu mstaafu, Cleopa David Msuya (aliyezikwa jana mkoani Kilimanjaro) kuelekea Kumbukizi ya Miaka 17 tangu kifo cha Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ikiandikwa na Mwandishi MGAYA KINGOBA.

Msuya anabainisha mambo makubwa aliyofanya Nyerere kwa Watanzania na nchi nyingine za Afrika katika uhai wake. Iliishia katika aya ambayo, Msuya anasema ‘… unapozungumzia suala la viwanda ambalo Serikali ya Awamu ya Tano ya Rais John Magufuli ni kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda kwa kuifi kisha katika uchumi wa kati, huwezi kukosa kumshirikisha, Msuya au kupata maoni yake kufahamu jinsi walivyosimamia viwanda wakati wa Mwalimu Nyerere’. Endelea…

Anasema hakuna muujiza wowote walioufanya, lakini baada ya kupewa uwaziri wa viwanda alikutana na wataalamu wake na kuchambua kinachopaswa kufanyika. “Kuwa na lengo la viwanda ni jambo moja, uwekezaji ni jambo lingine. Unaweza kuwa na fedha, lakini lazima ujenge uwezo. Wakati huo hatukuwa na fedha za kutosha,” anaeleza.

Msuya anasema wakati huo walikopa fedha ili kujenga na kuendesha viwanda hivyo na pia kutumia rasilimali za ndani pamoja na kushawishi wawekezaji kuwekeza na kujenga viwanda nchini. Kwa mujibu wa Msuya, wakati wao walikuwa na viwanda vikubwa 12 vya umma ndani ya miaka yake mitano ya uwaziri wa Viwanda (1975-1980). Anavitaja baadhi kuwa ni Mwatex, Mutex, Kilitex, Urafiki na Mufindi Paper.

Akizungumzia azma ya Rais Magufuli kuwa na Tanzania ya viwanda, Msuya anasema inawezekana, lakini anategemea kuwa Serikali ya Dk Magufuli (wakati huo) itafanya mambo kadhaa, ikiwamo kuweka fedha kimkakati ili kufanikisha azma hiyo na kushirikisha sekta binafsi na si tu Tanzania, bali hadi nje ya nchi.

Anasema nchi zilizoendelea kwa viwanda zikiwamo China, Japan, Ujerumani, Marekani na Uingereza zimechukua wawekezaji kutoka nje ya nchi zao ambao wanaungana na wazawa katika uwekezaji na masuala ya teknolojia. Katika hilo, anasisitiza pia suala la kuwaalika wawekezaji wanaokwenda katika eneo ambao wana ujuzi nalo na anatoa wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL).

“TBL wamepiga hatua kubwa kwa sababu wamepewa watu wenye ujuzi na uzoefu wa eneo la uwekezaji ambalo wamepewa la uzalishaji wa bia. Wamekifanya kiwanda cha Dar es Salaam kuwa cha kisasa, wamefungua kiwanda Mwanza na kujenga kiwanda kingine Mbeya.

“Kwa hiyo, utaona jinsi uwekezaji wao ulivyokuwa na manufaa makubwa. Hata Sigara wamefanya kazi nzuri, lakini tuna viwanda vya ngozi, hali zao zikoje…” anaeleza Msuya. Anaamini uongozi wa Rais Magufuli kwa kuwa una maono, utafanikiwa kusimamia vizuri azma ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda.

“Lazima uwe na maono na kuwe na ufuatiliaji wa karibu wa uongozi wa Taifa, bila ya hivyo mnaweza kukwama,” anasema. Msomi huyo wa uchumi anazungumzia pia, suala la elimu tangu wakati wa Mwalimu Nyerere hadi sasa, akibainisha kuwa baada ya Uhuru, Nyerere hakuwa na rasilimali za kutosha kuendesha elimu, lakini akatumia falsafa ya kupanga ni kuchagua; ndio maana kukawepo na kitu cha UPE (Elimu ya Msingi kwa Wote) kisha sekondari.

Awamu ya pili na ya tatu ya uongozi wa nchi zilifanya kazi ya upanuzi wa elimu ulioendelezwa katika Awamu ya Nne ambayo udahili ulikuwa mkubwa zaidi na wanafunzi wa elimu ya juu wakazidi kuongezeka vyuoni. “…kuna ongezeko kubwa la wanafunzi sasa, na hata fedha zimeongezeka kiasi kwamba sasa tunasikia na huko nako kuna ‘majipu.’ Lakini ni vyema wenye fedha walipe na wale wanyonge wasaidiwe,” anasema.

Hata hivyo, anatoa angalizo kwa wasomi ambao wengi wanazungumzia ajira serikalini. Anasema: “Msilalamike,
fursa zipo. Hata kulima vitunguu ni kazi yenye manufaa makubwa, angalia fursa ziko wapi… Unaweza kuangalia
fursa zilizopo katika nchi kama Comoro, Kenya ukatoa vitunguu vyako Mang’ola (Arusha) na kupeleka huko.”

Hivi karibuni, Rais Magufuli alitangaza kuhusu serikali yake kuhamia Dodoma ndani ya miaka minne na ushee iliyobaki katika muhula wake wa kwanza. Msuya anaeleza jinsi utawala wa Mwalimu Nyerere ulivyosimamia kuhamia Dodoma, ikiwamo kuanzisha Kura ya Maoni kupata maoni ya wananchi kuhusu azma hiyo.

Rais wa Awamu ya Tano, John Magufuli akiagana na Waziri Mkuu Mstaafu, Cleopa Msuya baada ya kumjulia hali nyumbani kwake Upanga, Dar es Salaam. (Picha Kutoka Maktaba)

“Hili (suala la kuhamia Dodoma) lilikuwa linakuja kila mara bungeni. Kwa hiyo ikaanzishwa kama ‘White Paper’, na wakati huo chombo chenye nguvu ni chama, hivyo likapelekwa katika chama, watu wote wakasema ‘Ndiyo’.
Ukaandaliwa Waraka wa Baraza la Mawaziri, ukapelekwa bungeni kwa ajili ya sheria ili uwepo utekelezaji wake,” anasema Msuya anayekiri kukwama kwa kuhamia Dodoma kutokana na uwezo mdogo wa serikali wakati huo.

“Ndipo ikaanzishwa CDA (Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu) ili iandae mpango. Akapewa, George Kahama. Akasukuma ramani, akaweka hivi na hivi. Waziri Mkuu Kawawa (Rashid Kawawa) akahamia huko, akawa na ofisi pale katika Boma la Ujerumani (ndio ofisi hadi leo njia ya kwenda Stesheni ya Reli). Sokoine pia alihamia pale baada ya Kawawa kutoka.

Nami na mke wangu na watoto tulihamia huko nilipopewa wadhifa huo,” anasema Anaongeza: “Lakini hali ya uchumi haikuwa nzuri, ingawa misingi ya jambo hilo ilikuwapo. Ikulu ya Rais ilijengwa, kukawa na chumba cha Baraza la Mawaziri, nyumba ya kuchukua marais wawili, Tamisemi, Tumetaa, Bunge likaanza pale ‘White House,’ baadaye likajengwa pale Msekwa.”

Kwa mujibu wa Msuya, Dodoma kumekuwa na maboresho makubwa ya miundombinu, umeme wa Gridi ya Taifa unapatikana, maji ni mengi, barabara nzuri za lami kuunganisha na mikoa mingine ikiwamo inayokwenda hadi Cape Town, Afrika Kusini, kujengwa kwa vyuo vikuu mbalimbali vya serikali na madhehebu ya dini.

“Naamini sasa Rais atatimiza ndoto zake kwa sababu kuna baadhi ya watu walikuwa mguu mmoja huku (Dar es Salaam) na mwingine kule (Dodoma)… Ametumia fursa kutimiza ndoto za wananchi,” alieleza.

Kuhusu siasa kwa ujumla, mwanasiasa huyo mkongwe aliyewahi kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa, anasema haridhishwi sana na uendeshaji wa siasa hasa zile za baadhi ya vyama vya upinzani nchini.

Anasema vyama hivyo vilitakiwa vitoe uongozi mbadala lakini vinakosa sifa hiyo, na kwamba havina programu
mbadala inayoeleweka.

“Kizuri kilichofanywa ni pale walipochimba na kuibua sakata la EPA, na serikali ilichukua hatua. Lakini hivi karibuni wamesusa kuingia bungeni? Hoja ni nini hasa?” Issue (suala) ni uwakilishi, je wanawakilisha mawazo ya watu waliowatuma kwa kugoma. Wanapaswa kuwa makini zaidi,” anasema.

Na katika hilo, anaweka wazi kwamba wakati wa kusaka maoni kwa ajili ya Katiba mpya, alipendekeza kuwa haina haja ya kuwa na vyama vingi (kwa maana ya idadi) na badala yake sheria itungwe kwamba chama ambacho katika Uchaguzi Mkuu kitashindwa kupata idadi fulani ya kura, basi kifutiliwe mbali “ili kubaki na vyama vichache, lakini vyenye kuwajibika kwa wananchi na vinavyokubalika na wananchi hao.”

Kwa Taifa, Mzee Msuya ambaye Novemba 4, 2016 alitimiza umri wa miaka 85, anavutiwa na hatua alizochukua  hadi, Rais Magufuli na anaona ushauri kwa Watanzania na serikali kwa ujumla, ikiwamo kujipanga upya akisema: “Tuliyumba kidogo na sasa tunapaswa kujikita katika vipaumbele.”

Anavitaja vipaumbele hivyo kuwa ni pamoja na kukusanya mapato kama anavyohimiza Rais Magufuli, kubana
matumizi kwa sababu fedha zilikuwa zinatumika kwa matumizi yasiyo ya lazima.

“Lingine ni mifumo lazima ilete matunda. Wote waliopewa madaraka lazima watekekeze, na wasiotekeleza wawajibike, yaani vitu haviendi wao wapo tu. Katika vitu vyote, uongozi ni muhimu,” anasema Mzee Msuya na kubainisha kuwa, fursa zipo nyingi nchini, kwani upo umeme wa kutosha, gesi, kiasi kwamba Tanzania karibuni itaanza kuuza ziada ya nishati kwa nchi jirani.

“Tutoke katika utamaduni wa kulalamika tuingie katika kufanya na kutenda. Iwe katika siasa, michezo, kanisani,
msikitini. Mungu atatoa katika kipindi hiki,” anasema na kusisitiza kuwa, fursa zipo nyingi na kubwa zinazoweza
kuwafanya Watanzania kuwa na uchumi imara.

“Fursa ni kubwa, kubwa, tunahitaji uongozi wenye mtazamo wenye kusisitiza katika vipaumbele. Viongozi wasaidie watu ili vitu vitekelezwe, wasiotekeleza waondolewe,” anasema Msuya na kubainisha kuwa, nchi zote zilizoendelea ni kwa sababu ya uongozi imara. Anatoa mfano wa Japan ya kuanzia kwa Jeneral Park, Malaysia, Singapore na Dubai.

“Watu wanataka maendeleo, Rais Magufuli (wakati huo) ameonesha mwanzo mzuri anaenda pamoja na watu. Tunachotaka ni matokeo. Tukiwa focus (malengo), vyombo vya habari vikaacha kuhangaika na vitu vidogo vidogo, nchi hii inaweza kusonga mbele. Kwa nini tushindwe,” anasema Msuya, msomi wa Chuo Kikuu cha Makerere kuanzia mwaka 1952 hadi 1955.

Msuya ni nani?
Alizaliwa Novemba 4, 1931 Chomvu, Usangi wilayani Mwanga mkoani Kilimanjaro. Alisoma Makerere na kisha kufanya kazi katika maeneo ya vijijini Tanzania kuanzia mwaka 1956 hadi 1964. Tangu mwaka 1964, alihudumu kama Katibu Mkuu katika wizara mbalimbali zikiwamo Maendeleo ya Jamii na Utamaduni, Ardhi Makazi na Maendeleo ya Maji, Fedha na Mipango na Fedha.

Alikuwa Waziri wa Fedha mwaka 1972 hadi alipoteuliwa kuwa Waziri wa Viwanda mwaka 1975. Baada ya miaka mitano ya kazi hiyo, aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu mwaka 1980 hadi Februari 1983, kabla ya kuwa Waziri wa Fedha tena kuanzia Februari 1983 hadi Novemba 1985.

Novemba 6, 1985 aliteuliwa kuwa Waziri wa Fedha, Uchumi na Mipango hadi Machi 1989. Machi 1989 hadi
Desemba 1990, alikuwa Waziri wa Fedha tena, kabla ya kuteuliwa kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara kuanzia 1990 hadi 1994.

Desemba 1994, Msuya aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu kwa mara ya pili, akiwa pia na wadhifa wa Makamu wa Rais. Alidumu hadi Novemba 1995, alipochaguliwa tena kuwa Mbunge wa Mwanga na kubaki bungeni hadi alipostaafu Oktoba 29, 2000.

Makala hii ilitumika kwa mara ya kwanza Septemba 2016

 

 

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button