Mtaalamu: Msongo wa mawazo huathiri zaidi wanawake

Dar es Salaam : MTAALAMU wa Saikolojia, Sophia Sanga amesema tafiti zinaonesha kwamba msongo wa mawazo huathiri wanawake karibu mara mbili zaidi kuliko wanaume.
Ameanisha kuwa miongoni mwa sababu ni kuwa na majukumu ya kulea watoto, changamoto za kifamilia, matatizo ya kifedha, na wakati mwingine shinikizo kutoka kwa jamii.
Akizungumza wakati akitoa mada katika hafla ya watumishi wanawake wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) jijini Dar es Salaam, Sophia amesema mwanamke mara nyingi hubeba majukumu mengi katika jamii kama kuwa mama, mlezi wa familia, mfanyakazi, na wakati mwingine kiongozi katika jamii, ambapo majukumu haya mengi yanaweza kumweka katika hatari zaidi ya kupata changamoto za afya ya akili.
Amesema pia wanawake hupitia mabadiliko ya homoni katika maisha yao, kama vile wakati wa ujauzito, baada ya kujifungua, na wakati wa kukoma hedhi.
“Mabadiliko haya yanaweza kuathiri hali ya hisia na afya ya akili na wakati mwingine mwanamke anaweza kujikuta akiwa na huzuni, hasira au kukosa usingizi bila sababu kubwa inayojulikana,” amesema.

Amesema katika zama za teknolojia na mitandao ya kijamii, wanawake wengi wanakutana na shinikizo la kuonekana kwa mwili wao ambapo wengine wanajilinganisha na picha wanazoona mitandaoni, na hivyo kujisikia hawaridhiki na miili yao inayoweza kusababisha matatizo ya ulaji, kujinyima chakula, au kujiona hawatoshi.
“Kwa hiyo ni muhimu sana jamii kutambua na kuzungumzia afya ya akili ya wanawake kwa uwazi. Wanawake wanahitaji msaada, ushauri, na mazingira salama ya kuzungumza kuhusu changamoto wanazopitia,” amesema.
Mgeni rasmi katika hafla hiyo Mkurugenzi wa MNH, Dk Delilah Kimambo amesema katika hafla hiyo zaidi ya Wanawake 1,500 wa MNH wamepewa mafunzo ya kukabiliana na msongo wa mawazo, kuweka mpangilio wa maisha ya familia na kazi na utunzaji wa fedha.
Dk Kimambo amesema kuwa hospitali ina jumla ya wafanyakazi 3,000 ambapo wanawake wanachukua zaidi ya asilimia 70 ya wafanyakazi hao hivyo ni muhimu kwao kuhakikisha wanatunza afya zao hasa akili.
“Tunapaswa kuwa na kauli nzuri kwa wagonjwa kwani wao wameletwa na matatizo hivyo tuwe sehemu ya faraja kwao na tunaona hapa Muhimbili wahuduma wanawake ndio wengi lakini ukienda kwenye suala la wanaotoa majibu yasiyofaa wanawake ndio wanaongoza, “ameeleza.
Amesema wanawake wana mchango mkubwa katika utoaji wa huduma na maendeleo ya hospitali hivyo ni muhimu kuzingatia maadili ya utoaji huduma.
Amewaambia wanawake hao kuwa ni muhimu kushirikiana na wanaume ili kuhakikisha wanajenga mazingira yenye usawa na ushirikiano.



