DAR ES SALAAM: MKURUGENZI wa Kinga wa Wizara ya Afya nchini Tanzania Dk Ntuli Kapologwe ameibuka na ushindi wa nafasi ya Mkurugenzi Mkuu wa Jumuiya ya Afya ya Nchi za Afrika Mashariki, Kati na Kusini (ECSA – HC), na kuwashinda wagombea kutoka nchi mbalimbali waliokuwa wakiwania nafasi hiyo, na ataongoza kwa muda wa miaka mitano.
Dk Ntuli anachukua nafasi hiyo kutoka kwa Profesa Yoswa Dambisya wa Uganda ambaye amehudumu kwenye nafasi hiyo kwa mihula miwili ndani ya miaka 10.
Soma zaidi: Dk Kapologwe ataka uwazi, uwajibikaji
Akizungumza mara baada ya kuhitimisha zoezi la uchaguzi huo, Waziri wa Afya, Jenista Mhagama amesema nafasi hiyo ilipotangazwa kwa mara ya kwanza jumla ya waombaji 47 waliwasilisha wasifu wao na kati yao saba walichaguliwa kuendelea baada ya mchujo wa awali.
Waziri Mhagama amesema mara baada ya usaili uliofanywa na Kamati ya Mkutano wa Makatibu Wakuu wa nchi wanachama, Dk Kapologwe alipata alama za juu zaidi na kuingia katika hatua ya mwisho pamoja na wagombea wengine wawili kutoka Kenya na Malawi.