“NILIKUWA nikiumizwa na habari za mazao yetu kushambuliwa na magonjwa, kama mnyauko lilininyima usingizi, nikiwa katika majukumu yangu ya kazi nilipitia vichwa vya habari katika vyombo vya habari kwamba Kagera ni mkoa wa mwisho yaani ni maskini nikajiuliza mkoa wetu utakuwaje maskini wakati kuna ardhi, mito, hali nzuri ya hewa?”
Hiyo ni kauli ya Fidelis Bashasha, Mkurugenzi wa Kampuni ya Global Agency iliyojikita katika kuzalisha mbegu za muda mfupi zitakazomkomboa mkulima wa mazao mbalimbali kama maharagwe, mahindi, soya, ngano na mtama.
Hatua hiyo inatokana na kuumizwa na Mkoa wa Kagera kutajwa katika umaskini. Aliamua kuacha kazi yake na kujikita katika uwekezaji wa kuzalisha mbegu za mazao.
Taaluma yake kubwa aliyosomea ni mifumo, kwa miaka mingi alijihusisha kubuni mifumo mbalimbali (APPs), lakini ameamua kuacha kazi yake na kuingia katika kilimo cha mbegu za mazao yanayoweza kustahimili ukame na kukua haraka ndani ya miezi mitatu.
Bashasha anasema haukuwa uamuzi rahisi kuacha kazi yake lakini aliamini kuwa mkoa ambao una mito, ardhi ya kutosha ni rahisi kufanya uwekezaji utakaokuwa mkombozi kwa wakulima na wakazi wa Kagera hasa katika kuwaepusha na changamoto ya mazao yao kushambuliwa na magonjwa.
Kwa sasa Bashasha kupitia kampuni yake ya Global Agency anazalisha mbegu zenye ubora ambazo zinatumiwa na wakulima ambazo ni mbegu za mahindi 5c627, soya, ngano, maharage ambazo zimeanza kutumiwa na wakulima wa Kata ya Bugorola, Kijiji cha Buchurago wilayani Missenyi. Lengo kubwa ikiwa ni kukidhi haja na kutoa mbegu bure kwa wakulima wa wilaya hiyo bila malipo.
“Mkoa wa Kagera unategemea kilimo kuondoa umasikini, huwezi kuzungumzia utajiri wa Kagera kama utajiweka nyuma katika masuala ya kilimo, kama tunaweza kufanikiwa kuzalisha mazao yetu kwa wingi na kwa ubora tunaweza kufanya Mkoa wa Kagera kupunguza umasikini kwa sababu tuna uwezo wa kuuza katika nchi za Afrika Mashariki,” anasema Bashasha.
Anasema kwa sasa tayari anafanya uwekezaji wa kuzalisha mbegu bora za mazao katika ekari 21,000, ekari 13,060 zimelimwa na anafanya umwagiliaji ambapo amezalisha tani 32 za mahindi na soya tani 90 huku akisema kuwa endapo serikali itamuunga mkono katika uzalishaji na uwekezaji shamba linaweza kuzalisha tani 17,000 kila msimu.
Anasema kwa sasa wilayani Missenyi wakulima waliokuwa wakichukua mbegu ya mahindi kutoka Zambia na Botswana tayari wameanza kunufaika na mbegu inayozalishwa katika wilaya hiyo na wanaofanya umwagiliaji tayari wamevuna bila changamoto yoyote ya mbegu hiyo.
Kupitia uwekezaji wake, tayari wananchi wa Missenyi wapatao 300 wameajiriwa kwa ajira za muda mfupi na muda mrefu, kipaumbele ikiwa ni vijana waliomaliza vyuo vya kilimo kupata ajira za kudumu ili miaka mitatu ijayo ajira za kigeni zipungue na mradi uendeshwe na wazawa ambao wamehitimu vyuo vya kilimo.
Nyuma ya pazia miaka mitano iliyopita alijaribu kilimo cha mazao katika uwekezaji wake lakini alipata hasara kwani kila akikaribia kuvuna mazao yalikuwa yakivamiwa na maji na yote kuzama lakini hakukata tamaa aliendelea kutafuta ufumbuzi mpaka sasa ambapo anafanya kilimo cha umwagiliaji na analima wakati wa kiangazi na kupata mbegu bora.
“Maisha hayahitaji kukata tamaa, nawashukuru viongozi wa benki na wa serikali ambao kila nilipokwama waliniambia nijaribu tena ili nitimize lengo nililokusudia, nilijaribu tena na tena kwa sababu huwezi kupata eneo lililoungana kuwekeza kama hakuna maji na sasa nimefanikiwa sina changamoto tena, ninachoomba ni serikali kuniunga mkono,” anasema Bashasha.
Bashiru Adadi, mhitimu wa SUA na mzaliwa wa Kijiji cha Buchurago, Kata ya Bugorola, anasema alikaa miaka minne bila kupata kazi lakini kwa sasa ameajiriwa na mwekezaji huyo hivyo anasaidia kutoa elimu ambayo pia inakifikia kijiji chake.
Anaamini hivi karibuni kama mwekezaji ataungwa mkono tatizo la kuagiza mbegu kutoka nje litaisha na fedha zitabaki nchini na mzunguko wa fedha utaongezeka.
Anasema kwa sasa wananchi wanazalisha kwa tija na mwekezaji anatoa nafasi ya wataalamu kuwafikia wakulima na kuwaelekeza juu ya kupanda mbegu bora na kuvuna mavuno mengi hivyo ajira yake haimnyimi nafasi ya kutoa huduma na elimu kwa wananchi wa kijiji chake alichozaliwa.
Naye Athuman Baltazal, mhitimu mwingine wa SUA na mtaalamu wa kudhibiti magugu, anasema uwekezaji wa kilimo cha kuzalisha mbegu umeleta mabadiliko makubwa kwa wakulima wa Wilaya ya Missenyi kwani wengi kwa sasa wanalima kilimo cha kitaalamu ukilinganisha na miaka ya nyuma.
Anasema huenda swala la mazao kushambuliwa na magonjwa likabaki historia kwani kumekuwa kukiibuka magonjwa yanayoshambulia mbegu za mazao ya wakulima lakini kwa sasa mbegu inayozalishwa na Global Agency wakulima wamevuna bila kupitia changamoto yoyote na furaha zaidi ni ajira na utaalamu wanaoupata kutoka kwa mwekezaji huyo.
Diwani wa Bugorola, Renovatus Rumanyika, anasema anafurahishwa jinsi wananchi walivyompokea mwekezaji na habari njema zaidi ni jinsi wananchi anaowaongoza katika kata hiyo hasa vijana wanavyochangamkia fursa ya kilimo kwa kupanda mbegu hizo zenye tija lakini ushiriki wao katika ajira za shambani.
Anasema huenda hivi karibuni umasikini uliowahi kutajwa kuwa kata hiyo ni ya mwisho kwa umasikini ikafutika kwani kwa sasa ujio wa mwekezaji huyo umetoa ajira na wananchi wamebadilika, wameanza kujenga nyumba za kisasa na kupata milo mitatu kwa siku.
Mkuu wa Wilaya ya Missenyi, Wilson Sakulo anasema kuwa ameshuhudia panda shuka za mwekezaji huyo wakati anaanza kuwekeza lakini ni miongoni mwa watu waliomtia moyo na sasa anashuhudia mabadiliko makubwa katika kilimo cha mazao mbalimbali ambacho anafanya mwekezaji huyo.
Sakulo anasema amekuwa shuhuda wa kupita katika mashamba ya wakulima baada ya mbegu kuanza kupatikana, hivyo kwa sasa anaamini hakutakuwa na mbegu kutoka nchi jirani kwa sababu wamekubaliana na wasambazaji wa mbegu waliokuwa wanaleta mbegu kutoka nje ya nchi kwamba wachukue mbegu kutoka kwa mwekezaji huyo kwa sababu ni mbegu ambayo inazalishwa kila mmoja akiiona na tayari imekubaliwa na wakulima wenyewe.
Anasema serikali inaendelea kuunga mkono jitihada za wawekezaji wanaotaka kuleta mabadiliko chanya kwa wananchi huku akiomba mwekezaji huyo kujenga kiwanda au kuingia ubia na wawekezaji wengine kujenga kiwanda cha kupaki mbegu hizo katika Wilaya ya Missenyi kuliko mbegu hizo kuzalishwa Missenyi na kwenda kupakiwa Arusha.
Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Abdulrahman Kinana, amefanya ziara ya kutembelea shamba hilo la kuzalisha mbegu na kukiri kuridhishwa na mbegu zinazozalishwa katika shamba hilo. Kinana aliambatana na viongozi mbalimbali wa serikali na chama.