DAR ES SALAAM: CHUO Kikuu Cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kimesema kitafanya uzinduzi wa Mfuko wa Maendeleo wa Ali Hassan Mwinyi wa MUHAS (AHMMEF) ukiwa ni mpango wa mkakati unaolenga kusaidia maendeleo endelevu ya elimu na tafiti chuoni hapo.
Akizungumza chuoni hapo, Makamu Mkuu wa MUHAS, Profesa Appolinary Kamuhabwa amesema uzinduzi huo utafanyika Februari 28, 2025 katika Kituo cha Umahiri wa Magonjwa ya Moyo na Mishipa ya Damu, Kampasi ya Mloganzila Dar es Salaam, lengo kumuenzi Rais wa Pili Tanzania, Ali Hassan Mwinyi.
“Mfuko utatoa msaada wa kifedha wa kudumu kwa miradi bunifu, programu za kitaaluma, na ustawi wa wanafunzi na wanataaluma. Lengo kuu ni kuhakikisha kuwa MUHAS inaendelea kuwa chuo bora cha elimu ya afya na sayansi shirikishi, utoaji huduma za afya na utafiti,” amesema Prof Kamuhabwa.
Aidha, Prof Kamuhabwa amesema uzinduzi huo utaenda sambamba na uzinduzi wa kongamano la kila mwaka la kumuenzi Mwinyi ambapo litakuwa jukwaa linalowakutanisha wataalamu wa sekta ya afya na elimu kujadili masuala yanayohusu maendeleo ya sekta hizo na mustakabali wake.
“Kongamano hilo litahusisha wasilisho kuu la kumbukumbu na kuthamini mchango wa mkuu wa kwanza wa chuo cha MUHAS, na Rais wa Pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika masuala mbalimbali, ikiwa ni pamoja na MUHAS; mijadala yenye lengo la kuimarisha mifumo ya afya na elimu ameongeza Prof Kamuhabwa.
Amesema kongamano hilo litatumika pia kurejesha vazi rasmi la mkuu wa kwanza wa chuo kwa familia: “Katika heshima ya pekee kwa Hayati Ali Hassan Mwinyi, MUHAS itarudisha vazi rasmi la Mkuu wa Chuo aliloloweka akilia wakati wa Mahafali hapo chuoni kwa familia yake. Tendo hili litakuwa kumbukumbu ya mchango wake wa kipekee katika maendeleo ya elimu”.