UKARABATI wa kivuko cha Mv Kazi kinachofanya safari zake kati ya Magogoni na Kigamboni mkoani Dar es Salaam unakaribia kukamilika.
Kivuko hicho kiliondolewa kwenye maji mwishoni mwa Februari mwaka huu baada ya kufikia muda wake wa ukarabati.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA), Lazaro Kilahala alisema kilichokuwa kinasubiriwa ilikuwa ni vifaa.
“Sehemu kubwa ilikuwa ni kufunga vifaa vipya vya injini, gia boksi na mifumo mipya ya injini, kwa hiyo zile kazi ambazo zilikuwa zinaweza kufanyika kabla ya vifaa hivyo ilikuwa zaidi ya asilimia themanini na zote zilifanyika ikiwemo kazi za kuondoa vipande vya bati ambavyo vimeharibika na kupiga rangi upya,” alisema Kilahala.
Mwakilishi wa Kampuni ya Songoro Marine wanaofanya ukarabati wa kivuko hicho, Hamad Aweso alisema ukarabati wa kivuko hicho umefikia hatua nzuri.
Kivuko cha Mv Kazi kina uwezo wa kubeba abiria 800 na magari 22 sawa na tani 170 kwa wakati mmoja.
Hivi sasa eneo la Magogoni Kigamboni limebaki na vivuko viwili vinavyotoa huduma kikiwemo kivuko cha Mv Magogoni na Mv Kigamboni, ambavyo kwa sasa vinasaidiana na vivuko viwili kutoka kampuni ya Azam Marine kutoa huduma eneo hilo.
Ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) inaeleza kuwa chama hicho katika kipindi cha miaka mitano ijayo, kitahakikisha miundombinu ya usafirishaji na uchukuzi inaboreshwa kwa lengo la kufungua fursa za kiuchumi na kijamii katika maeneo ya mijini na vijijini.
Katika ilani hiyo CCM inaeleza kuwa inatambua kuwa uendelezaji wa miundombinu ya uchukuzi ni hitaji la msingi katika kuchochea na kuwezesha maendeleo ya sekta za kiuchumi na kijamii.
Mpango wa Taifa wa Maendeleo unaeleza kuwa Tanzania kuna maziwa makuu manne ya Victoria, Nyasa, Tanganyika na Rukwa na katika maeneo hayo fursa za uvuvi wa samaki, ufugaji wa samaki, madini ya chumvi, utafutaji wa gesi na mafuta, kilimo cha mwani, utalii wa fukwe, usafiri na usafirishaji.