MKOA wa Mwanza umeanza kampeni kuhamasisha mama wajawazito kuhudhuria kliniki ili kufahamu afya yao na hivyo kuwaepusha na matatizo yasiyoyalazima wakati wa kujifungua.
Hayo yamebainishwa Alhamis na Mratibu wa elimu ya afya kwa umma Mkoa wa Mwanza, Denis Kashaija alipokuwa akizungumza na HabariLEO.
Alisema lengo la kuanzisha kampeni hiyo ni kudhibiti viashiria hatari kwa wanawake wajawazito ili kuwa na uzazi salama.
Alisema viashiria hivyo hatari kwa wajawazito ni mimba katika umri mdogo ambao ni chini ya miaka 18, kuwa na upungufu mkubwa wa damu, kovu la kupasuka analokuwa nalo mjamzito kutokana na uzazi uliotangulia.
Kashaija aliongeza kusema kuwa viashiria vingine hatari kwa wajawazito ni kifafa cha mimba na mimba za zaidi ya tano hivyo alitoa wito kwa jamii kufahamu ili kuweka uangalizi mkubwa kwa makundi hayo kwa lengo la kuokoa maisha.
Akitoa takwimu alisema kati ya mwezi Januari hadi Machi mwaka huu kulikuwa na wajawazito 1,837 kuwa na mimba ya zaidi ya tano.
Vilevile wajawazito wengine 172 walikuwa na shinikizo la juu la damu, huku 335 wakiwa na tatizo la kovu la kupasuka wakati wa mimba ya nyuma.
Aliendelea kusema kuwa pia wajawazito 547 walikuwa na tatizo la upungufu wa damu.
Alisema kampeni inafanyika katika maeneo yote ya huduma za afya ili kuwezesha jamii kufahamu uzazi salama wa afya zao.
Kashaija alisema kuwa hatua hiyo itawafanya wajawazito na watoto kuwa salama.