Mwigulu: Tusiikwamishe serikali sensa ya watu na makazi

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba amewataka Watanzania wasiikwamishe serikali katika kazi ya sensa ya watu na makazi ili kuiwezesha kupata takwimu sahihi zitakazosaidia kuendesha uchumi kwa kupanga na kufanya mipango ya maendeleo kwa usahihi.

Aliyasema hayo alipozungumza katika mkutano ulioendeshwa kwa njia ya mtandao wa Zoom kujadili umuhimu wa sensa katika maendeleo ya taifa ambapo alisema takwimu sahihi zinasaidia serikali kufanya uamuzi sahihi katika masuala ya maendeleo na kwa usawa.

“Tunapokuwa na takwimu sahihi tunaendesha uchumi kwa kupanga, tunapokuwa na takwimu za uongo tunaendesha uchumi kutokana na matukio, mnafanya mambo bila kupanga kwa hiyo sensa itatusaidia kuwa tunafanya makadirio sahihi kwa bajeti zinazofuata na kufanya mgawanyo sahihi wa maendeleo kwa wananchi,” alisema.

Advertisement

Alitoa mfano wa hasara za kutokuwa na takwimu sahihi ni kuanzishwa kwa shule za sekondari katika kila kata ambayo iliongeza mzigo wa gharama kwa serikali kuhakikisha shule zinakuwa tayari lakini baadaye baadhi ya shule hizo zilikosa wanafunzi kutokana na kata hizo kuwa na wanafunzi wachache. Alieleza kuwa kama kungekuwa na takwimu za kutosha, shule hizo zingejengwa kulingana na wingi wa wanafunzi katika kata husika.

Mwenyekiti wa Kamati ya Ushauri ya Kamati Kuu ya Sensa, Dk John Jingu ambaye pia ni Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu alieleza kuwa sensa ni muhimu kwa serikali na mtu mmoja mmoja katika kufanikisha shughuli za uchumi na maendeleo hasa kunapokuwa na takwimu sahihi za watu katika makundi mbalimbali.

Alisema kupitia sensa serikali itajua idadi ya watu, umri, jinsia na hali zao mnyambuliko ambao utawezesha serikali kupanga mipango ya maendeleo kwa kujiamini kulingana na taarifa zitakazopatikana.

“Kama watoto wameongezeka kwa serikali maana yake ni kwamba ikajenge madarasa ya kutosha, huduma za afya na kadhalika. Tukipata wazee ni wengi basi serikali itahakikisha huduma zinazotakiwa kwa wazee zinapatikana, kama kina mama ni wengi na pengine wana changamoto serikali itaweza kuamua kwa usahihi,” alisema Jingu.

Mjadala huo pia ulishirikisha viongozi wa dini akiwemo Mufti Mkuu na Shehe wa Tanzania, Abubakar Zubeir ambaye alieleza umuhimu wa sensa na kuwataka Waislamu kujitokeza kuhesabiwa kwani hilo ni jambo jema wala haliharibu Uislamu kama wengine wanavyopotosha.

Alisema hakuna mali popote katika dini panaposema sensa haifai isipokuwa ni jambo kubwa ambalo limesaidia kukua na kuendelea kwa dini ya Kiislamu na katika vitabu vingi. Mufti alisema masuala ya kuhesabiwa yalifanyika tangu wakati wa mtume walipotafuta idadi ya watu hivyo siyo kitu kibaya kama wengine wanavyopotosha na serikali imefanya jambo jema kufanya sensa ya watu na makazi mwaka huu.

Mtazamo huo wa Mufti uliungwa mkono na Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT), Fredrick Shoo ambaye alieleza kuwa imani kwamba sensa ni kitu kibaya ni potofu inayopaswa kupuuzwa kwani kwa Wakristo suala la kuhesabiwa ni suala lililozungumzwa hata katika Biblia. Alitolea mfano wakati wa kuzaliwa Yesu, Mariam na Yusuf walipoamriwa kwenda Galilaya kuhesabiwa.

“Kama jambo la sensa lingekuwa kinyume na Mungu angeweza kuwafanya Mariam na Yusuf wasitii amri ya Kaisari, Mungu anataka watawala wajue idadi ya makundi yao, napenda kuwaondoa hofu na hayo mawazo potofu waumini wote wa Kikristo na Watanzania wote wajue kuwa sensa siyo kitu kibaya wala haina nia ovu,” alisema Askofu Shoo.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *