Maisha wenye ulemavu kuboreshwa Z’bar

RAIS wa Zanzibar na Mgombea wa Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Hussein Ali Mwinyi, amewaomba watu wenye ulemavu nchini kumpa kura katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, huku akiwaahidi kuboresha zaidi maisha yao katika awamu yake ya pili ya uongozi.
Akizungumza na makundi ya watu wenye ulemavu katika ukumbi wa Idriss Abdul Wakil, Kikwajuni – Unguja, Dk. Mwinyi alisema serikali yake tayari imefanya mambo mengi kwa ajili ya kundi hilo, na kwamba wanaweza kutarajia hatua zaidi zitakazoinua ustawi wao endapo atachaguliwa tena.
“Naomba mniunge mkono kwa kunipigia kura tarehe 29 Oktoba. Asibaki mtu nyumbani. Pia tuwaunge mkono wagombea wetu wote wa CCM – kuanzia Dk. Samia Suluhu Hassan, wabunge, wawakilishi hadi madiwani,” alisema Dk. Mwinyi katika mkutano huo uliopambwa na shamrashamra. SOMA: Mwinyi: Hakuna atakayedhulumiwa fidia
Baada ya kusikiliza changamoto mbalimbali zinazowakabili watu wenye ulemavu ikiwemo ukosefu wa ajira, kutoshirikishwa katika ngazi za maamuzi, upungufu wa vifaa saidizi, na miundombinu isiyo rafiki Dk. Mwinyi aliahidi kuchukua hatua madhubuti kuzitatua.
Alisema serikali yake itaendeleza programu za mafunzo, uwezeshaji na mikopo nafuu kwa watu wenye ulemavu, sambamba na kuhakikisha haki zao zote zinalindwa na kutekelezwa ipasavyo. “Sera yetu tayari inataka majengo yote ya serikali na miundombinu izingatie mahitaji ya watu wenye ulemavu. Pia visaidizi kama viti vya magurudumu, mafuta maalum ya watu wenye ualbino, na viungo bandia havina ushuru,” alieleza Dk. Mwinyi huku akishangiliwa.
Akijibu maombi ya kuanzishwa kwa kitengo maalum cha huduma za afya kwa watu wenye ulemavu, Dk. Mwinyi alisema serikali itafungua vituo maalum katika hospitali mpya za Mnazimmoja na Binguni mara tu zitakapokamilika, ili kuhakikisha huduma za matibabu zinapatikana bila ubaguzi au vikwazo vya kifedha.
Vilevile, aliahidi kuongeza nafasi za ajira na uteuzi serikalini kwa watu wenye ulemavu, ili nao washiriki moja kwa moja katika maamuzi na maendeleo ya taifa. Aidha, alisema serikali itaendelea kuimarisha ustawi wa kiuchumi wa kundi hilo kwa kutoa mikopo isiyo na riba na mitaji ya kuendeshea shughuli zao za kiuchumi.
Mkutano huo ulihudhuriwa pia na Mke wa Rais wa Zanzibar, Mama Mariam Mwinyi; Katibu wa Kamati Maalum ya NEC, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo CCM Zanzibar, Khamis Mbeto Khamis; na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dk. Mohamed Said Mohamed Dimwa, ambao walimnadi Dk. Mwinyi.



