BARAZA la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limetembelea na kufanya ukaguzi kwenye kiwanda cha A One Product and Bottles Limited kilichopo Kibaha mkoani Pwani kinachojihusisha na urejelezaji wa chupa za plastiki zilizotumika.
Akizungumza na Uongozi wa kiwanda hicho kwa niaba ya Kaimu Mkurugenzi Wa Uzingatiaji na Utekelezaji, Mhandisi wa Mazingira NEMC Juhudi Mwashibanda amepongeza juhudi zinazofanywa na kutoa wito kwa kiwanda hicho kuzingatia Sheria na Kanuni za Usimamizi wa Mazingira.
SOMA: NEMC yatoa neno utunzaji bahari
“Niwapongeze kwa hatua hii kubwa ya kuweka miundombinu bora ya Urejelezaji wa chupa za plastiki naamini hatua hii itasaidia kupunguza taka za chupa za plastiki mitaani, pia nitoe wito kwa kiwanda hiki kuzingatia Sheria na Kanuni za Usimamizi wa Mazingira” amesema Mhandisi Mwashibanda.
Mhandisi Mwashibanda amehimiza wazalishaji wote ambao bado hawajaweka miundombinu ya Urejelezaji wa chupa za plastiki kufanya hivyo ili kupunguza uchafuzi wa Mazingira.
Naye Afisa Usalama, Afya na Mazingira kiwanda cha A One Product and Bottles Limited, Aureus George amesema baada ya kupokea maagizo kutoka NEMC, wamefanikiwa kuweka miundombinu ya kisasa inayoweza kurejeleza chupa za plastiki zaidi ya Tani 9 kwa saa moja huku wakilenga kuokoa na kutunza Mazingira.
Itakumbukwa kuwa Februari mwaka huu Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) lilitoa maagizo kwa wazalishaji wa chupa za plastiki zenye rangi zilizoisha matumizi kuweka miundombinu wezeshi ya kurejeleza chupa hizo ili kutunza Mazingira.
Hivyo ukaguzi huo unalenga kufuatilia Utekelezaji wa maagizo hayo..
Comments are closed.