One Acre Fund kuchagiza usambazaji pembejeo za ruzuku

IDADI ya wakulima wanaonufaika na pembejeo zinazosambazwa na Kampuni ya One Acre Fund Tanzania Ltd katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini inatarajia kuongezeka kutoka 160,000 wa msimu wa kilimo uliopita hadi 220,000 katika msimu ujao wa 2022/2023.

Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Amar Khalid Hamad alitoa taarifa hiyo hivi karibuni wakati wakizindua duka kubwa la pembejeo katika Kijiji cha Kalenga wilayani Iringa, mkoani Iringa uliofanywa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Halima Dendego.

Katika msimu ujao wa kilimo, Hamad alisema wakulima hao watanufaika na tani 15,000 za pembejeo za ruzuku zitakazosambazwa kupitia programu yao ya pembejeo za mkopo na pembejeo za malipo taslimu kwa kupitia maduka yao 40 yaliyoko katika mikoa hiyo.

Advertisement

Alisema One Acre Fund inajivunia kuwa na programu ya msingi ya kufikisha kwa wakulima pembejeo zenye ubora wa hali ya juu katika vijiji karibu na makazi ya wakulima.

Akifungua duka hilo la Kalenga, Mkuu wa Mkoa wa Iringa aliipongeza kampuni hiyo ambayo imepanga pia kusambaza miche ya miti milioni mbili ikiwemo ya matunda, mbao na inayotumika kuboresha udongo ili kuongeza kipato cha mkulima.

Dendego alisema katika msimu wa kilimo wa 2022/2023 serikali imepanga kutoa ruzuku ya mbolea kwa wakulima kwa lengo la kupunguza gharama ya mbolea sokoni ili kuongeza uzalishaji na tija katika kilimo, kuimarisha usalama wa chakula na kuongeza upatikanaji wa malighafi za viwanda vya ndani.

Alisema utekelezaji wa mpango huo wa ruzuku utakaowanufaisha wakulima wote watakaosajiliwa.

 

/* */