‘OUT isambae halmashauri zote’

'OUT isambae halmashauri zote'

CHUO Kikuu Huria Tanzania (OUT), kinapaswa kisambae katika halmashauri zote 184 zilizopo nchini, ili kila Mtanzania mwenye kiu ya elimu aipate.

Meya wa Halmashauri ya Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, Songoro Mnyonge, amesema hayo alipokuwa akimwakilisha Mkuu wa Wilaya hiyo, Saad Mtambule katika Baraza Kuu la Tisa la Wafanyakazi wa OUT.

Mnyonge amesema kutokana na ongezeko kubwa la watoto wanaozaliwa kila kukicha, OUT inapaswa kupanuka, alitoa mfano kuwa hospitali ya Mwananyamala kila siku watoto 100 huzaliwa, hivyo chuo hicho kinachoendesha elimu ya masafa kinapaswa kujitanua nchi nzima, ili kuhimili ongezeko hilo la watoto.

Advertisement

Amesema kwa mfumo huo wa elimu masafa, wananchi watajiendeleza kirahisi huku wakiendelea na shughuli zao za kila siku.

Awali Makamu Mkuu wa OUT, Prof. Elifas Bisanda amesema amepitia takwimu mbalimbali na kuona idadi ya wanafunzi katika shule za msingi tangu hayati Dk Rais John Magufuli, alipoagiza itolewe elimu bure kuanzia darasa la kwanza hadi la saba.

” Mwaka huu wanafunzi watakapofanya mtihani wa darasa la saba ni 1,387,448. Walioko darasa la sita ni 1,369,453. Walioko darasa la nne ni 1,691,102 na walioko darasa la tatu ni 1,881,323,” alisema Profesa Bisanda.

Amesema kwenye website ya Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania ( TCU), inaonyesha uwezo  wa vyuo vikuu vya Tanzania wa kudahili wanafunzi ni 150,000.

Amesema kutokana na takwimu hiyo, wanafunzi waliohamasika na elimu bure watakapomaliza kidato cha nne watakuwa ni wengi kuliko miaka iliyopita hivyo nafasi ya pekee ya elimu ya juu ni kujiunga na OUT.

” Idadi ya watoto watakaokuwa na uwezo wa kuingia vyuo vikuu itakuwa ni kubwa mara tatu au nne ya uwezo wa vyuo vikuu vilivyopo nchini vya serikali na binafsi.

” Kwa hiyo miaka minne au mitano ijayo kiimbilio pekee la watoto kwenda kusoma elimu ya juu itakuwa ni Chuo Kikuu Huria,” amesema.

Almesema chuo hicho hakina mipaka ya kudahili wanafunzi, kwani kwa kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano( Tehama), kina uwezo wa kuchukua wanafunzi milioni moja.