Pambano la Nassib lakwama Nigeria
BONDIA wa ngumi za kulipwa hapa nchini Nassib Ramadhan, amesema kuwa pambano lake dhidi ya Rilwan Oladosu kutoka Nigeria limeota mbawa baada ya mpinzani wake kugomea kupima uzito.
Pambano hilo la raundi 10 lisilokuwa la ubingwa lilipaswa kupigwa leo Machi 5, 2023 katika ukumbi wa Police College Ikeja, jijini Lagos, Nigeria.
Akizungumza na HabariLEO, bondia huyo amesema alisema kwa upande wake maandalizi ya pambano hilo yalikuwa yamekamilika, alikuwa akisubiri kupima uzito, lakini mpinzani wake akashindwa kufika ukumbini.
“Nashukuru Mungu kila kitu kilienda sawa kwa upande wangu, lakini mpinzani wangu hakuwa tayari kupima uzito kwa kile alichodai hakuna mkataba wa yeye kucheza pambano hilo.
“Napenda kuwashukuru mashabiki wangu waliokuwa wakinipa sapoti licha ya kuwa mbali na nyumbani naomba wasikate tamaa narudi kujipanga kwa ajili ya mapambano mengine lengo langu ni kuipeperusha bendera ya Tanzania,” alisema Ramadhan.



