Papa Francis amtunuku nishani Mtanzania
BABA Mtakatifu Papa Francis, amemtunuku Padri Richard Mjigwa wa Tanzania, nishani ya Msalaba wa Kanisa na Papa kutokana na huduma ya mawasiliano ya Kanisa kupitia Redio Vatican Idhaa ya Kiswahili.
Padri Mjigwa pia anahudumu katika Baraza la Kipapa la Mawasiliano kupitia Idhaa ya Kiswahili ya Redio Vatican ni Mtanzania wa pili kutunukiwa tuzo hiyo, baada ya miaka 6 tangu Mtanzania wa kwanza aliyehudumu katika baraza hilo, Thabita Janeth Mhella kutunukiwa tuzo hiyo Septemba, 2016.
Padri Mjigwa ambaye ni Mwanashirika wa Shirika la Damu Azizi, alikabidhiwa tuzo hiyo na Mhariri Mkuu wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano la Kipapa, Dk Andrea Tornielli kwa niaba ya Papa Francis, kufuatia juhudi zake za kuhudumia jamii katika kueneza sauti na miongozo ya Papa katika lugha ya Kiswahili kupitia Redio Vatican kwenye mataifa yanayozungumza lugha hiyo.
Padri Mjigwa aliyezaliwa Tanzania mwaka 1964, alianza shughuli ya huduma ya uandishi wa habari kama mshirika mwaka 1994 hadi 1999 na baadaye kuanza rasmi katika Idhaa ya Kiswahili ya Redio Vatican kuanzia mwaka 2008 hadi sasa.
Katika hatua nyingine, Padri Mjigwa kwa niaba ya Idhaa ya Kiswahili ya Redio Vatican alipokea tuzo ya maadhimisho ya miaka 30 ya idhaa hiyo, ambayo ilianzishwa rasmi Septemba 27, 1992. Tuzo hiyo ameipokea wakati muafaka ambapo lugha ya Kiswahili imeendelea kutambulika duniani kama lugha kuu mojawapo ya mawasiliano.
Utangazaji katika lugha ya Kiswahili kwenye Redio Vatican ulianza mapema mwezi Novemba 1961.