Pongezi TRA, tuendelee kulipa kodi kwa maendeleo

AKIHUTUBIA Bunge wiki iliyopita wakati akihitimisha shughuli za Bunge la 12, Rais Samia Suluhu Hassan alisisitiza suala la kulipa kodi kwa hiari.
Alisisitiza kwamba angependa kuona wafanyabiashara, wawekezaji na wananchi wanaelimishwa na kutambua kwamba kodi ndiyo msingi wa maendeleo ya nchi, na hivyo, wawezeshwe kulipa kodi bila kutumia mabavu.
Na katika kufikia azma hii, Rais Samia alieleza kuwa serikali imeimarisha mifumo ya kielektroniki ya ukusanyaji mapato, udhibiti wa mianya ya kupoteza mapato, kuanzisha Jukwaa la Kodi na Uwekezaji, na kuijengea uwezo Mamlaka ya Mapato Tanzania na mamlaka nyingine za ukusanyaji mapato ya serikali.
Kutokana na jitihada hizo na nyingine, haikushangaza kuona kuwa makusanyo ya kodi chini ya TRA yamezidi kuongezeka na kwa mara nyingine yamevunja rekodi.
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa juzi, TRA imeweka rekodi kwa ukusanyaji wa mapato kwa kukusanya Sh trilioni 32.29 katika mwaka wa fedha 2024/2025.
Mapato hayo yamevunja rekodi tangu kuanzishwa kwake mwaka 1996/1997. Takwimu zinaonesha kuwa katika robo hii ya nne iliyoanza Aprili mpaka Juni, TRA ilipaswa kukusanya Sh trilioni 7.84, lakini mpaka Juni 30, ambayo ndiyo siku ya mwisho katika mwaka wa fedha, ilikusanya Sh trilioni 8.22.
Kutokana na makusanyo hayo ya mwisho, TRA imeweka rekodi ya kukusanya Sh trilioni 32.29 kwa mwaka wa fedha Tanzania Bara na Zanzibar.
Kwa mujibu wa Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda, awali lengo ilikuwa kukusanya Sh trilioni 31.65 lakini sasa wamevuka lengo kwa asilimia 16.7, ufanisi ni mkubwa kwa asilimia 103, ikiwa ni mafanikio makubwa na rekodi ni kubwa tangu kuanzishwa kwa mamlaka hiyo mwaka 1996/1997.
Zinatajwa sababu nyingi kutokana na mafanikio hayo ikiwamo ya utekelezaji kwa vitendo wa maagizo ya Rais Samia na viongozi wengine, ya kutaka kodi ikusanywe kwa staha na kila anayestahili kulipa kodi afanye hivyo.
Tunaipongeza TRA kwa kusimamia kwa vitendo utekelezaji huo wa agizo la Rais Samia ambalo limewezesha makusanyo haya makubwa. Hii ina maana kuwa ulipaji wa kodi kwa hiari unalipa, na unastahili kuendelezwa.
Tunasema hivyo kwa sababu wafanyabiashara na watu wengine wanaostahili kulipa kodi wakielimishwa na kufahamu wajibu wao, watalipa kodi kwa hiari na hivyo kuchangia katika maendeleo ya nchi.
Tunaamini TRA inao uwezo wa kukusanya mapato zaidi ya Sh trilioni 32.29 za sasa, kwa sababu mazingira ya ulipaji kodi yamezidi kufanywa kuwa rafiki na hivyo zile tabia za kulipa kodi kwa shuruti zimepungua kama si kuondoka kabisa.
Hata hivyo, bado kuna eneo la TRA kuendelea kulifanyia kazi ambalo ni kuongeza wigo wa walipakodi ili makusanyo yazidi kuongezeka na Watanzania wengi zaidi wachangie katika kugharimia maendeleo yao kwa fedha zao.
Tumeona jinsi Serikali ya Rais Samia inavyotekeleza miradi mingi ya maendeleo kwa fedha zake na hizi zitapatikana endapo kila anayestahili kulipa kodi atafanya hivyo. Tuendelee kulipa kodi kwa maendeleo bila kusubiri shuruti.