Rais Samia aelekeza Polisi kukomesha watu kupotea

DODOMA: RAIS wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amelielekeza Jeshi la Polisi nchini kuongeza kasi na juhudi katika kupambana na matukio ya uhalifu, hususan vitendo vya kupotea kwa watu ambavyo vimekuwa vikilalamikiwa na wananchi.

Rais Samia ametoa agizo hilo leo wakati akilihutubia Bunge jijini Dodoma kwaajili ya kuhitimisha shughuli za Bunge la 12, huku akielezea mafanikio yaliyofikiwa na serikali katika kipindi hiki cha uongozi kabla ya uchaguzi mkuu ujao.

Katika hotuba yake, Rais Samia amelipongeza Jeshi la Polisi kwa hatua nzuri katika kudhibiti uhalifu nchini, akibainisha kuwa kasi ya kuwabaini, kuwakamata na kuwafikisha mahakamani wahalifu imeongezeka kwa kiasi kikubwa.

“Serikali imeendelea kuliimarisha Jeshi la Polisi kwa kuboresha mazingira ya kazi na kuongeza miundombinu,” alisema Rais Samia.

“Hadi sasa, vituo vya polisi 472 vimejengwa nchi nzima, makazi ya askari yameboreshwa, na vitendea kazi kama magari na pikipiki vimenunuliwa kwa ajili ya kazi za utawala na operesheni,” amesema Rais Samia.

Rais Samia amesema suala la haki za binadamu kwa wafungwa, serikali imeendelea kuboresha huduma za malazi, mavazi na chakula kwa wafungwa, kulingana na hali ya uchumi inavyoimarika.

Katika hatua nyingine, Rais Samia amelitambua Jeshi la Magereza kwa kazi nzuri ya urekebishaji wa wafungwa na kulinda haki zao, ambapo amesema serikali imepandisha vyeo maafisa waandamizi na askari 14,733 wa jeshi hilo, na pia askari wapya 3,404 wameajiriwa ili kupunguza uhaba wa rasilimali watu.

“Hii ni pamoja na kuwapatia magari kwa ajili ya kazi, kuongeza magereza mapya manane, na ujenzi wa hospitali kuu ya kanda ya Magereza hapa Dodoma unaoendelea vizuri,” ameongeza Rais Samia.

Kwa upande wa matumizi ya teknolojia, serikali imefanikisha magereza 66 kutumia mfumo wa Mahakama Mtandao (TEHAMA), ambao unasaidia kusikiliza kesi bila ulazima wa kuwasafirisha wafungwa hadi mahakamani.

Kuhusu Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Rais Samia amesema serikali imeendelea kuliimarisha jeshi hilo kwa kujenga vituo vipya vitatu vilivyokamilika, na vituo vinane vinaendelea na ujenzi, vituo vya zamani vimekarabatiwa, na magari 12 ya zimamoto pamoja na boti mbili za uokoaji kwa ajili ya Bahari na Ziwa Victoria vimenunuliwa.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button