Rais Samia aipongeza Stars, aipa mil 700/-

RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan ameipongeza na kuipatia Timu ya Taifa ya Tanzania shilingi Milioni 700 kwa kufuzu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika(AFCON 2025 nchini Morocco, baada ya kuifunga Guinea goli 1-0 kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Dk. Damas Ndumbaro amesema hayo na kuwahakikishia wachezaji na viongozi wa timu hiyo kuwa fedha hizo tayari zimishawekwa katika akaunti ya Wizara hiyo.

Fainali za AFCON 2025 zitakazofanyika Morocco kuanzia Desemba 21, 2025 hadi Januari 18, 2026.
SOMA: Hatma Taifa Stars kufuzu AFCON leo
“Tukiwa katika majonzi na kazi ikiendelea katika kuwatafuta ndugu zetu ambao tunaamini bado wako hai kufuatia kuporomoka kwa jengo eneo la Kariakoo, ninawapongeza vijana wetu Taifa Stars kwa ushindi na kufuzu kushiriki Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025. Mmeandika historia kwa Taifa letu, ikiwa ni mara yetu ya nne kufikia mafanikio haya makubwa katika kipindi cha zaidi ya miaka arobaini,” amesema Rais Samia kupitia ukurasa wake wa X.

Pia amepongeza Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF), Benchi la Ufundi na Watanzania wote kwa kuendelea kuipenda, kuithamini na kuipa hamasa Timu ya Taifa.
“Baada ya ushindi huu, sasa tujikite katika maandalizi mazuri zaidi kwa mashindano yajayo,” amesema mkuu huyo wa nchi.
Tanzania imeshika nafasi ya pili katika kundi H wakati wa hatua ya kufuzu ikikusanya pointi 10 nyuma ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo iliyomaliza kwa kuongoza kwa pointi 12.
Hii ni mara ya nne kwa Tanzania kufuzu fainali za AFCON huku ikifuzu mara tatu mfululizo 2019, 2023 na 2025 na mara ya kwanza ilikuwa 1980.