Rais Samia amepata tuzo sita za kimataifa

DODOMA — Serikali imetangaza mafanikio ya kitaifa na kimataifa ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa mwaka huu wa 2025, ikiwa ni pamoja na tuzo sita za kimataifa na shahada tano za heshima kutoka vyuo mbalimbali.
Akieleza mafanikio hayo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Rais Samia ametambuliwa kwa juhudi katika afya, miundombinu, sanaa, utalii, na diplomasia ya uchumi. Pia ametajwa kuwa kiongozi wa kwanza Afrika kupokea Tuzo ya Global Gates Goalkeepers.
“Mheshimiwa Rais amekuwa Mwalimu wa subira, kielelezo cha ujasiri, ustahimilivu na alama ya matumaini kwa kizazi hiki na kijacho,” alisema Majaliwa kwa msisitizo mkubwa wa heshima.
Tuzo hizo ni pamoja na tuzo ya Babacar Ndiaye (miundombinu), Pyne Africa (utalii), na African Leadership Award (sanaa). Shahada za heshima alizopokea ni kutoka vyuo vya India, Korea, Uturuki, SUZA na UDSM.
Majaliwa alisema heshima hizo ni ushahidi wa uongozi wake imara unaotambuliwa duniani, na kuwa Watanzania wanapaswa kuuenzi kwa moyo wa kizalendo.