“NIKIANZA kuangalia tulikotoka, ni miaka 30 tangu Azimio la Beijing, hili Azimio la Beijing liliona kuna shida ya wanawake katika uongozi na tukiwa tunaadhimisha miaka 30 toka Azimio la Beijing lilipotolewa, lazima tujitafakari na tujitathmini tulikotoka, tuliko na tunakokwenda.”
“Niseme tu wazi kwamba, tunakoenda ni bora zaidi katika misingi kwamba, tulikotoka mwanamke alikuwa hapewi nafasi, lakini kwa uhamasishaji na utoaji elimu, watu wameanza kuelewa kwamba mwanamke katika jamii tangu katika ngazi ya familia, anatoa mchango mkubwa.”
Ndivyo anavyosema Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN), Asha Dachi anapozungumzia maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani inayoadhimishwa kesho Machi 8, 2025.

Dachi anazungumzia namna anavyoiona nafasi ya mwanamke katika uongozi nchini hasa baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuingia madarakani na kuonesha imani kubwa kwa mwanamke katika utekelezaji wa majukumu.
Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani hulenga kutambua mchango wa mwanamke katika jamii na kuimarisha na kulinda haki zake hata katika utekelezaji wa majukumu.
Kaulimbiu ya maadhimisho ya Siku ya Mwanamke Duniani mwaka huu ni: ‘Wanawake na Wasichana 2025 Tuimarishe Haki, Usawa na Uwezeshaji’ ikilenga kumwezesha mwanamke kwa kuweka usawa wa kimajukumu na kuzingatia haki.
Nchini Tanzania, Rais Samia ambaye ni kinara wa utetezi na ulinzi wa haki na usawa wa binadamu ukiwamo wa wanawake, amekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha nafasi ya mwanamke katika vyombo vya uamuzi
inaongezeka tangu alipoingia madarakani Machi 19, 2021.
Katika hafla ya kuwaapisha majaji aliowateua mwaka 2022 iliyofanyika Ikulu ya Chamwino, Dodoma, Rais Samia
alisema anapata msukumo zaidi kuteua majaji wanawake kutokana na weledi wao katika kazi, juhudi na uadilifu.
Anabainisha kuwa moja ya sababu za kupungua kwa lawama za wanachi dhidi ya mahakama ni kuongezeka kwa idadi ya majaji wanawake katika Mahakama ya Tanzania. Takwimu za Mahakama ya Tanzania kuhusu uwakilishi wa wanawake katika ngazi mbalimbali zinaonesha hatua kubwa iliyofikiwa na pia safari ndefu iliyopo.
Inaelezwa hadi Machi 8, 2024 takwimu zinaonesha kuwa majaji wa Mahakama ya Rufani walikuwa 35. Kati yao, wanaume walikuwa 22, sawa na asilimia 63 na wanawake walikuwa 13, sawa na asilimia 37. Kuhusu majaji wafawidhi wa Mahakama Kuu, walikuwa 26 huku wanaume wakiwa 17, sawa na asilimia 65 na wanawake tisa sawa na asilimia 35.
Idadi ya majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania ilikuwa 105 wanaume wakiwa 67 sawa na asilimia 64, huku wanawake wakiwa 38 sawa na asilimia 36. Takwimu zinaonesha pia kuwa naibu wasajili walikuwa 78. Kati ya hao,
wanaume walikuwa 40, sawa na asilimia 51 na wanawake walikuwa 38 sawa na asilimia 49.
Kwa upande wa mahakimu wakazi, idadi yao ilikuwa 1,126. Wanaume walikuwa 567, sawa na asilimia 50 na wanawake wakiwa 559, sawa na asilimia 50.
Kwa mujibu wa wadau wa haki za binadamu na usawa wa kijinsia, takwimu hizo zinabainisha pengo baina ya wanawake na wanaume linaendelea kupungua katika Mahakama ya Tanzania hasa kwa wakati huu ambao Rais Samia ameonesha wazi imani yake kwa wanawake na anaweka mkazo katika kuongeza nafasi zao kwenye uongozi kupitia teuzi zake.
Kama haitoshi, Tanzania inashuhudia wanawake wakiongoza taasisi mbalimbali za serikali na kubwa zaidi, wanaonesha tija katika utendaji wao. Kuhusu suala hili, Dachi anasema katika masuala ya uongozi katika nyakati hizi wanawake ‘wameamka’, wanasoma na wanaona nafasi yao katika uongozi ni muhimu na kubwa.
“Lakini ukija katika uongozi, watu wamekuja kusoma zaidi na kuona kwamba mwanamke ana nafasi kubwa katika
uongozi na mwanamke akiaminiwa anajitoa zaidi pengine ni zaidi ya jinsia nyingine.” “Inawezekana kwa muda mrefu wamekuwa wakiwaamini upande wa jinsia moja na upande mwingine wa jinsia ukaonekana ni dhaifu, kumbe
huu ni upande wenye nafasi na uwezo mkubwa kwenye uongozi,” anasema.
Dachi anasema ukweli huo unadhihirishwa na mfano halisi wa Rais Samia ambaye amekuwa kiongozi bora wa nchi
anayekubalika ndani na nje ya nchi na kuwa mfano wa kuigwa na wanawake wengi. Anasema Rais Samia amejenga hamasa na kujituma zaidi kwa wanawake.
Uchunguzi wa mwandishi umebaini kuwa, Rais Samia anapoteua wanawake katika nafasi mbalimbali za uongozi, wanawake hao hujiona wanapaswa kumuunga mkono kwa kufanya kazi vizuri zaidi ili kutimiza matarajio yake.
“Na sisi tunapoteulilwa katika nafasi mbalimbali, …tunakuwa na hamasa na ari kubwa ya kutimiza kwa sababu kama kinara wako anafanya kwa moyo mkuu na kila mmoja anaona bila kushurutishwa maana yake maendeleo ya nchi hii baada ya kuingia awamu hii ya sita inayoongozwa na ‘Mama’ mwenye moyo wa mama, lakini upande wa pili ni
kiongozi shupavu na ushupavu wake umeonekana kwa miradi mikubwa aliyoisimamia.”
“…Kimsingi, hakuna kilichoshindikana, hakuna kilichosimama, hilo kwetu viongozi wanawawake limekuwa mfano mzuri wa kuigwa kama njia ni nzuri ya kwetu wanawake wote kupita ili na sisi tufanya vizuri zaidi,” anasema Dachi.
Anasema anaona dalili njema ya kuwa na nafasi nusu kwa nusu ya uongozi katika kipindi kijacho cha uongozi wa Rais Samia kutokana na namna anavyoongeza idadi ya viongozi wanawake kwenye safu yake.
Anasema hali hiyo inaongeza ari kwa mabinti walioko shuleni na vyuoni wanaofanya vizuri wakiwa na nia ya kuwa viongozi wa baadaye na anaamini kutakuwa na kizazi bora cha viongozi wanawake huko mbeleni kwani wanaonesha uwezo tangu wakiwa shuleni na vyuoni.
Anawashauri mabinti ni wajifunze kwa watangulizi wao waliopo sasa akiwemo Rais Samia wanavyofanya vizuri na kwa kuwa wameshaanza kufanya vizuri kwenye masomo yao wakaze uzi, waendelee kuonesha uwezo wao na kwa kufanya hivyo ushindani utakuwa uko sambamba na utakuwa hauangalii jinsia bali uwezo wa mtu.
Anawataka wajiandae kuwa viongozi katika nyanja zote kwa sababu si kwamba mtoto wa kike akisoma ni lazima aje awe kiongozi kwenye taasisi za serikali au siasa bali hata kwenye maeneo mengine ikiwemo kwenye kujiajiri.
Anasisitiza kuwa umefika wakati wa kudhihirishia ulimwengu kuwa mwanamke ni kiongozi na mwokozi wa mwanamke mwenzake na si adui.
“Tulikuwa tunaaminishwa kwamba ‘adui wa mwanamke ni mwanamke mwenzie, hapana tumebadilisha hiyo ‘slogan’ (kauli mbiu) tunasema ‘rafiki wa mwanamke ni mwanamke mwenzie’ na tutakuja kuidhihirisha hiyo kwenye Uchaguzi Mkuu (Novemba mwaka huu) na tunahakikisha kwamba tunampa (Rais Samia) mitano tena,” anasema.
hi
I was BROKE and desperate… now I make $3,000+ weekly from my couch! Just 30 days ago, I was stuck in a dead-end job, living paycheck to paycheck. Then I found this secret method—and everything changed Anyone can do this in their free time. Spots are LIMITED! Don’t miss out!
Join now➤➤ http://Www.WorksProfit7.Com