RC Geita ataka mikakati sensa migodini
MKUU wa Mkoa wa Geita, Martin Shigella, amewaagiza viongozi wa mitaa, vijiji na kata kwa ushirikiano na makarani wa sensa kuhakikisha wanawaandaa wachimbaji wadogo, ili kufanikisha sensa kwenye maeneo ya migodini.
Shigella ametoa maelekezo hayo alipokuwa akizungumuza na watumishi wa halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale mkoani hapa, pamoja na makarani wa sensa wilayani humo wanaoendelea na semina kuelekea sensa.
Amesema Mkoa wa Geita una maeneo mengi ya wachimbaji wadogo, hivyo ni lazima uandaliwe utaratibu mzuri wa mapema, ili kuepuka sintofahamu pindi mawakala wa sensa watakapowasili kutekeleza majukumu yao.
“Ni vizuri watendaji wetu wa vijiji na kata pamoja na madiwani, tufanye maandalizi mapema kwenye yale mazingira, maana usipowaandaa wachimbaji wadogo, ukaenda saa sita usiku kwenye machimbo unawaambia nimekuja kuwahesabu sensa hawatakuelewa.
“Kwa hiyo tuwashirikishe mawakala wa sensa walioko kwenye vile vituo, tuwashirikishe wamiliki wa leseni, kwa sababu wachimbaji wale wadogo wamejumuishwa kwenye leseni za watu Fulani,” amesema na kuongeza:
“Ili usiku wa tarehe 22 kuamukia tarehe 23 Agosti makarani watakapokwenda kwenye maeneo ya machimbo, wapewe ushirikiano, wamalize kuhesabu kabla ya saa 12 alfajiri, ili kukicha anayetakiwa kwenda kuchimba aende bila kucheleweshwa.”
Shigella amezitaka halmashauri kuzingatia maslahi ya makarani wa sense, ili waweze kulipwa kiwango sahihi na kwa wakati sambamba na kuwaandalia mazingira ya ulinzi na usalama kipindi chote cha sensa.