RC Mara apongeza wachimbaji madini

WATANZANIA 387 wameungana na kuendesha mgodi wa uchimbaji mdogo wa dhahabu wa Isaranilo, Buhemba, mkoani Mara na sasa wamejijengea soko la madini kwa Sh milioni 375, mambo ambayo yamepongezwa na Mkuu wa Mkoa huo, Meja Jenerali Suleiman Mzee.

Hayo yamedhihirika katika ziara inayofanywa na kiongozi huyo kwenye migodi tofauti, ili kujiweka katika nafasi nzuri inayolenga kumjengea kupokea taarifa ya sekta ya madini mkoani humo.

“Imefurahisha ujenzi huu, ingawa mmeanza kutumia baadhi ya maeneo jitahidini  mmalizie na mzingatie maelekezo niliyowapa, ili  huduma muhimu zipatikane ndani ya jengo,”alisema Meja Jenerali Mzee.

Hata hivyo hakupenda uchomaji wa awali wa dhahabu kufanywa kwa kutumia mkaa, akaagiza wapelekewe njia mbadala, iliyo bora na yenye kuhifadhi mazingira.

Makazi na mazingira ya wachimbaji hao pia hayakumfurahisha kiongozi huyo, ambaye aliwataka kutumia umoja wao kuyaboresha, kwa sababu ni miongoni mwa mambo yanayoweza kudhoofisha au kuboresha afya zao.

Mkuu wa Wilaya ya Butiama, Mwalimu Moses Kaegele, akimkaribisha Mkuu wa Mkoa kwenye mkutano huo alisema wachimbaji hao wamekuwa miongoni mwa vyanzo vikuu vya mapato ya Halmashauri hiyo, kwamba hupata kati ya Sh milioni 3 hadi 4 kwa wiki.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wachimbaji hao, waliomba kuwekewa mfumo mzuri wa kulipa tozo tofauti zikiwamo za serikali, ili waweze kutunza na kukuza mitaji.

Samwel Ojoro alitaka wajengewe hospitali kubwa na shule bora zisizopungua tatu, kwamba eneo hilo lina wakazi wengi ambao wanastahili huduma bora za kijamii.

Tumsifu Yusufu alitaka zinapobuniwa tozo mpya, elimu itolewe kwa wananchi, ili kuwe na uelewa wa pomoja na hivyo kusababisha utayari wa kulipa tozo husika bila usumbufu.

Meja Jenerali Mzee aliahidi kuzungumza na viongozi wa madini ngazi ya mkoa na viongozi wa wachimbaji hao  haraka, ili kupatia ufumbuzi hoja zao.

Habari Zifananazo

Back to top button