NAIBU Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma amesema vyombo vya habari vina jukumu la kuhakikisha vinaripoti habari za uchaguzi mkuu ujao kwa haki ili wananchi wapate taarifa sahihi.
Akizungumza jijini Dodoma wakati akifunga mkutano wa siku mbili wa vyombo vya utangazaji nchini uliondaliwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Mwinjuma amesema vyombo hivyo ni silaha kuu, bila hivyo demokrasia inaweza kuzama.
Amesema kupitia vyombo hivyo wananchi wanapata taarifa sahihi za wagombea zinazowawezesha kufanya maamuzi kwa mustakabali wa nchi hivyo vina umuhimu katika uchaguzi ujao wa Oktoba mwaka huu.
“Nimesikia katika mkutano huo wa siku mbili mmejadili masuala ya msingi kuhusu umuhimu wa vyombo vya utangazaji, Sheria na kanuni za uchaguzi Mkuu, mchango wa vyombo vya utangazaji, nawapongeza wote kwa kuchangia mada zilizowasilishwa.
“Nawahakikishia milango ya msaada wetu iko wazi kuhakikisha wote watakaohitaji tushirikiane katika sekta ya habari na utangazaji kwa maendeleo ya Taifa letu,”alisema.
Meneja wa huduma za Utangazaji wa TCRA Mhandisi Andrew Kisaka amesema mkutano huo umehudhuriwa na jumla ya washiriki 528 wa maudhui ya mtandaoni, redio na televisheni kutoka mikoa mbalimbali.
“Tumejifunza mada mbalimbali na kufanya baadhi ya mijadala tumepata matumizi sahihi ya Kiswahili, akili Mnemba, rasimu ya mkakati wa kukuza maudhui ya ndani. Tunatengeneza rasimu kuhakikisha tunakuza rasimu hapa nchini ili kuimarisha maudhui ya ndani.
“Tumetumia mkutano huu kufanya tathmini ya maazimio 18 tuliyofanya katika mkutano wa mwaka jana,”amesema.